2013-02-06 10:55:44

Siku ya Kupinga Vitendo vya Ukeketaji Kimataifa


Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 6 Februari 2013 inaadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Kimataifa ya Kupambana na vitendo vya ukeketaji vinavyodhalilisha utu na heshima ya wanawake na wasichana sehemu mbali mbali za dunia. Siku hii iliwekwa na Umoja wa Mataifa hapo Desemba, 2012 ili kupiga rufuku mila na tamaduni zote zinazoendeleza vitendo vya ukeketaji.

Haya ni matokeo ya mjadala mkubwa uliochukua muda mrefu katika medani za kisiasa na kidiplomasia, hadi kufikia muafaka huu. Hizi ni mila na tamaduni ambazo zimepitwa na wakati.Kuna baadhi ya nchi Barani Afrika kama vile. Burkina Faso, Benin, Niger, Pwani ya Pembe na Mali ambazo bado mila na tamaduni hizi zinaendelezwa kwa kiwango cha hali ya juu.

Lengo la Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha kwamba, hakutakuwepo tena na vitendo vya ukeketaji duniani, ifikapo mwaka 2015. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna wanawake, wasichana na watoto zaidi ya millioni 140 ambao wamekeketwa. Kila mwaka kuna wanawake na wasichana zaidi ya millioni tatu wanaokabiliwa na vitisho vya kukeketwa sehemu mbali mbali za dunia.

Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, hadi sasa kuna mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana, lakini bado kuna haja ya kuendelea kuwa makini kwani hivi ni vitendo vinavyofanyika kwa uficho na siri kubwa. Wanawake wenyewe wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukataa kushiriki katika vitendo vya ukeketaji, jambo linalohitaji Jamii kuhamasishwa na elimu ya jamii kuendelea kutolewa.







All the contents on this site are copyrighted ©.