Vatican na Italia yazindua Maadhimisho ya Miaka 84 ya Mkataba wa Laterano; uliotenganisha
Kanisa na Serikali!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Siku ya Jumatatu jioni, tarehe 4 Februari
2013, amemshukuru Rais Giorgio Napolitano wa Italia kwa zawadi kubwa ya Tamasha la
Muziki kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 84 ya Mkataba wa Laterano. Amewashukuru
wanamuziki wa "Flying Angels Foundation" ambao wamekuwa mstari wa mbele
katika kusaidia shughuli mbali mbali za kijamii.
Anasema, muziki ni kielelezo
makini cha majadiliano ya imani kati ya mwanadamu na Muumba wake; mwaliko na changamoto
ya kutubu na kumwongokea Mungu, daima akitumaini huruma na upendo ambao Mwenyezi Mungu
amekuwa akimwonesha mwanadamu katika hija ya maisha yake. Baba Mtakatifu anabainisha
kwamba, hakuna jambo lolote lile linaloweza kumtenga mwanadamu na upendo wa Mungu,
kama anavyo andika Mtakatifu Paulo kwa Warumi. Upendo huu unajionesha kwa namna ya
pekee kwa njia ya Yesu Kristo.
Muziki huu umesheheni tunu msingi za kijamii
zinazofumbatwa katika uhuru na usawa; sanjari na mapambano dhidi ya kifo, changamoto
kwa waamini kuwa na matumaini ya maisha ya uzima wa milele baada ya kifo.
Kwa
upande wake, Rais Giorgio Napolitano amemtakia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita, afya njema wakati huu wanapozindua kwa pamoja maadhimisho ya Kumbu kumbu ya
miaka 84 tangu Mkataba wa Laterano uliopotiwa sahihi kati ya Serikali ya Italia na
Kanisa Katoliki. Kumekuwepo na ushirikiano mwema kati ya Serikali ya Italia na Kanisa
Katoliki, kwa ajili ya mafao ya wengi, kila upande ukiheshimu na kuthamini mchango
unaotolewa kwa ajili ya wananchi wa Italia.
Rais Napolitano amekiri kwamba,
miaka saba ya uongozi wake, imekuwa kweli ni ya shida na taabu, si tu kwa Italia,
bali ni mwelekeo wa dunia nzima, lakini pia imekuwa ni fursa kwa viongozi hawa wawili
kushirikishana uzoefu na mang'amuzi ya maisha yao kwa kusikilizana kwa dhati. Majadiliano
yao ya mara kwa mara yamelenga zaidi na zaidi katika kudumisha misingi ya haki, amani,
mafao ya wengi, utu na maadili mema.