Kanisa linapania kuwekeza katika "vijiwe vya vijana" kama sehemu ya mkakati wa Uinjilishaji
mpya!
Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni, tarehe 6 Februari
2013 anatarajiwa kufungua mkutano mkuu wa Baraza hili, kwenye kikao cha wazi, kitakachowashirikisha
wadau mbali mbali wanaojishughulisha na utume na shughuli za kichungaji kwa vijana
wa kizazi kipya. Mkutano huu utafanyika kwenye Ukumbi mkubwa wa Chuo Kikuu cha LUMSA
hapa Roma.
Mkutano unapania
kuangalia masuala mbali mbali yanayogusa utamaduni na lugha ya vijana wa kizazi kipya,
ambao wengi wao wanapatikana katika Mitandao ya Kijamii.
Mada zinazotarajiwa
kujadiliwa ni pamoja mwingiliano wa kijamii miongoni mwa vijana; vijana wanaoishi
katika mitandao ya kijamii, lugha na ibada yao. Wajumbe watapata fursa ya kujadili
kwa undani zaidi kuhusu imani miongoni mwa vijana, hapa vijana watatoa ushuhuda wa
imani yao kadiri ya maisha yao na shughuli mbali mbali ambazo zimewasaidia kukuza
na kuimarisha imani hii licha ya kinzani na migogoro mbali mbali wanayokabiliana nayo
katika hija ya maisha ya ujana.
Wajumbe pia watajadili mbinu mkakati wa kuwaelimisha
vijana katika vionjo vyao. Mwishoni, ratiba inaonesha kwamba, wajumbe hawa watajadili
kwa kina na mapana kuhusu imani kwa ujumla na mapambano katika utamaduni. Baraza la
Kipapa la Utamaduni, litajadili pia mada zitakazojadiliwa kwenye mkutano wake mkuu
ujao.
Baraza la Kipapa la Utamaduni katika utekelezaji wa mikakati yake ya
kichungaji kwa Mwaka 2013, linapenda kuwekeza zaidi katika maisha na utume wa vijana
hasa kwenye “Vijiwe vyao” ili waweze kupata fursa ya kuimarisha imani na matumaini
yao kwa Kanisa, kama njia ya ujenzi wa utamaduni wa mawasiliano na urafiki kati ya
vijana wa kizazi kipya na Kanisa. Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza
la Kipapa la Utamaduni, wakati wa kuwasilisha tema itakayofanyiwa kazi na Baraza lake
katika mkutano mkuu unaoanza hapo tarehe 6 hadi 9 Februari, 2013, aliambatana na viongozi
waandamizi kutoka katika Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na vijana, ambao wametoa
ushuhuda kuhusu maisha na utume wao katika ulimwengu wa vijana mamboleo, wanaopatikana
kwa wingi katika Majukwa ya Mitandao ya Kijamii. Vijana hao kutoka Italia na Madagascar,
wanaosoma kwenye Vyuo Vikuu vya Italia wanabainisha kwamba, katika hija ya maisha
yao ya kiimani, wamebahatika kushuhudia matukio mbali mbali yaliyogusa undani wa maisha
yao, kiasi kwamba, yameacha chapa ya kudumu kama njia ya ushuhuda wa kujenga urafiki,
upendo na mshikamano katika hija ya maisha ya kiroho miongoni mwa vijana. Hii
sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na
kimwili. Ni kweli kabisa kwamba, kuna umati mkubwa wa vijana unaopatikana katika Majukwa
ya Mitandao ya Kijamii, lakini pia kuna mamillioni ya vijana ambao bado wanaendelea
na maisha yao ya kila siku pasi na kuguswa na mitandao hii. Kumbe, Kanisa linapaswa
kuwa na mwelekeo mpana linapowahangaikia vijana katika hija ya maisha yao ya kila
siku: kwa kuwatafuta kwenye Majukwaa ya Mitandao ya Kijamii bila kusahau kwamba, bado
kuna wengine wako “Vijiweni” kama kawaida!. Jamii ijitahidi kufahamu ulimwengu unaowazunguka
vijana, badala ya kubakia wakielea juu juu bila kuzama katika maisha, matumaini, kinzani,
changamoto na matarajio yao kwa siku za usoni. Vijana wanamshukuru Baba Mtakatifu
kwa kujimwaga katika Mitandao ya Kijamii, lakini Kanisa bado linawajibika kuwekeza
zaidi katika mitandao ya Kijamii ili kuweza kukutana na vijana wanaoendelea kujitosa
huko wakiwa na sababu mbali mbali, ili waweze kukutana nao, hatimaye, kuwamegea cheche
za imani zitakazowasha na kukoleza imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa lijitahidi
kufahamu lugha ya vijana wa kizazi kipya na kuifanyia kazi, kwani ni lugha inayogusa
undani wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Matumizi ya Mitandao ya Kijamii miongoni
mwa Vijana wa kizazi kipya ni fursa ya kukutana na watu mbali mbali na hivyo kuanza
kujenga mahusiano katika medani mbali mbali za maisha. Mitandao inapunguza umbali
na vikwazo ambavyo kwa miaka mingi vijana walikumbana navyo katika maisha yao! Hapa
ni mahali pa kujimwaga kisawa sawa na kwamba, watu wanatafuta majibu ya haraka na
yenye kusheheni kweli za Kiimani kutoka katika Kanisa. Umefika wakati kwa Mama
Kanisa kuonesha ule umahiri wa kuiwezesha Imani kutembea katika mitandao ya Kijamii,
ili vijana waweze kufaidika na maendeleo haya ya teknalojia ya mawasiliano na habari
kama sehemu ya mchakato wa kukua katika imani, matumaini na mapendo.