Wananchi wengi wa Syria wanatamani kuona haki, amani na utawala wa sheria vinaheshimiwa
nchini humo!
Vita na kinzani za Kijamii zinazoendelea nchini Syria zinapelekea watu wasiokuwa na
hatia kuendelea kupoteza maisha yao. Umefika wakati kwa wahusika wa pande zote mbili
zinazosigana nchini humo kuweka silaha chini na kuanza mchakato wa majadiliano ya
kisiasa ili haki, amani na utulivu viweze kutawala tena nchini Syria.
Taarifa
za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya watu 60,000 wamekwisha kupoteza
maisha kutokana na vita nchini Syria. Kuna watu wengine zaidi ya millioni moja wamelazimika
kuyakimbia makazi yao na kwa sasa hawana makazi maalum. Hali ya ulinzi na usalama
nchini Syria ni tete kutokana na ukweli kwamba, watu wengi wanamiliki silaha kali
zinazotishia maisha ya watu. Ni kwa njia ya majadiliano ya kisiasa, Syria inaweza
kupata ufumbuzi wa mgogoro wake.
Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na
Dr. Haytham Al-Manna moja ya wanaharakati wa kutetea haki msingi za binadamu alipokuwa
anazungumza na viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, kwenye Makao yake mjini
Geneva, hivi karibuni. Ni ndoto ya wananchi wengi wa Syria kwamba, nchi yao siku moja
itakumbatia demokrasia kwa kutambua kwamba, ni nchi ambayo ina tofauti kubwa za kidini
na kikabila.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linajiandaa kuadhimisha Mkutano
wake mkuu, Mwezi Oktoba, Korea ya Kusini, kwa kujikita zaidi katika masuala ya haki
na amani.