Sakata la Gesi Mtwara limefikia patamu, wananchi tugange yajayo!
Ifuatayo ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania aliyoitoa kama sehemu ya utaratibu
wake wa kuzungumza na Watanzania kila mwisho wa Mwezi. Katika hotuba hii anazungumzia
pamoja na mambo mengine kuhusu vurugu za kupinga gesi kusafirishwa toka Mtawara na
mchakato wa kupanga mji wa Mtwara. Ndugu Wananchi; Kama ilivyo ada naomba tuanze
kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha
kuzungumza kwa mara nyingine kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina
ya Rais na wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi. Siku ya leo nitazungumzia safari
yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia. Pia nitazungumzia ujenzi wa bomba la kusafirisha
gesi asili kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Safari za Kikazi Nje ya Nchi
Ndugu
Wananchi; Safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na manufaa
makubwa kwa nchi yetu. Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina
ya nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi wakubwa wenye nia thabiti ya kuja kuwekeza
hapa nchini. Pia tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa ushirikiano.
Mpango wetu wa sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka 2010. Mpango ule ulitusaidia
sana kuboresha huduma za maji katika miji ya Utete mkoani Pwani na Mpwapwa mkoani
Dodoma.
Katika mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika
Davos, Uswizi, tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza juhudi zetu za kuleta
mapinduzi ya kijani ili tujihakikishie usalama wa chakula na kupunguza umaskini vijijini
na kukuza uchumi wa nchi yetu. Aidha, tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala
wa kuanzishwa kwa programu kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya
upatikanaji wa umeme. Naamini programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa kuheshimu kauli
na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi za Afrika zilizo Kusini mwa
Jangwa la Sahara.
Ndugu Wananchi; Nchini Ethiopia tulishiriki
katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao cha
African Peer Review Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala bora ya
Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa. Kwa jumla hatuna mahali tuliponyooshewa
kidole kuwa tunafanya vibaya. Tumepongezwa katika mambo mengi na tumepewa ushauri
kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna budi kuyaboresha. Nilipata nafasi ya kusema
ambayo niliitumia kufafanua baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa. Niliwashukuru
na kuahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa. Tathmini ya nchi yetu ilipitishwa kwa
kauli moja. Vurugu za Kupinga Gesi Kusafirishwa Kutoka Mtwara Ndugu wananchi; Kama
mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya Ilala hapa Dar es
Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka
Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam. Karibu na mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika
maandamano mjini Mtwara kupinga ujenzi wa bomba hilo. Katika maandamano yale na baadaye
kwenye kauli za wanasiasa na wanaharakati yakatolewa madai kuwa gesi hiyo itumike
kwa maendeleo ya Mtwara na kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam yafanyike
Mtwara. Pia, zilitolewa shutuma nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa kwa miaka mingi
imewasahau na haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa bomba hilo ni muendelezo
wa hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na wanaharakati ni kama vile ziliongeza mafuta
kwenye kaa la moto na kuuchochea mpaka kukatokea matukio yaliyotusikitisha na kutshtua
sote. Baadhi ya ndugu zetu wamepoteza maisha na mali za watu na Serikali kuharibiwa.
Ndugu Wananchi; Katika hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka
2013, tarehe 31 Desemba, 2012, nililisemea jambo hili. Leo mwezi mmoja baadae, napenda
kusisitiza mambo mawili. Kwanza kwamba, si kweli kuwa Serikali inapuuza Mikoa ya
Kusini. Na pili, kwamba kujenga bomba la kuipeleka gesi Dar es Salaam hakuinyimi
Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya kunufaika na gesi iliyopo Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Serikali imefanya, inafanya na ina mipango ya kufanya mambo mengi mazuri kwa ajili
ya kuleta maendeleo katika Mikoa ya Mtwara na Lindi. Ipo mipango ya kuboresha miundombinu,
huduma za kiuchumi na kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
viwanda vikubwa na vidogo. Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Mstaafu,
Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto Rufiji maarufu kama Daraja la
Mkapa. Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali katika safari ya kutatua matatizo ya usafiri
ya Mikoa ya Kusini. Serikali ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi
wa barabara za lami kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma.
Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia kuimaliza. Tulikamilisha ujenzi
wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja hadi Nangurukuru. Mwaka 2009 tukaanza ujenzi wa
barabara ya kilomita 56 kutoka Somanga hadi Ndundu (darajani). Ujenzi wa kilometa
36 za mwanzo ulienda vizuri. Bahati mbaya ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho umechelewa
sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa kufanya kazi hiyo kufariki.
Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata mtikisiko kiasi na kusababisha kazi kutotekelezwa
kwa kasi tuliyoitarajia. Sasa mambo yametengemaa na kazi inaendelea kwa kasi nzuri.
Matumaini yetu ni kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Hali kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa alituachia jukumu la kumaliza
ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na ujenzi wa barabara ya lami kuanzia
Mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Tumelikamilisha Daraja hilo na ujenzi wa barabara ya lami
kutoka Masasi hadi Mangaka umekamilika. Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda Songea
na kwenda Darajani umefikia mahala pazuri. Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka Tunduru
hadi Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa. Kama mambo yataenda sawa miezi mitatu
ijayo mjenzi atapatikana. Wakati huo huo ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo hadi
Songea – Mbinga na Namtumbo – Tunduru unaendelea. Hivyo basi, kwa barabara ya “Mtwara
Corridor” kazi iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda Mbambabay ambayo tutaifanya wenyewe
kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja – Nangurukuru na Somanga – Ndudu na Daraja la Umoja.
Ndugu
Wananchi; Ipo pia mipango ya kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili iweze
kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji wa gesi baharini, kuhudumia na kuvifanyia
matengenezo vyombo vinavyotumika katika utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi.
Pia iweze kuhudumia shughuli za kiuchumi zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na
zilizopo sasa. Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale Mtwara tarehe 25
Julai, 2011 waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe mahali pa kuhudumia vyombo vyote
vinavyofanya shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta katika pwani ya
Afrika ya Bahari Kuu ya Hindi. Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari iwe bandari
huru. Niliwakubalia bila ya kusita na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa na kutangazwa
rasmi kuwa bandari huru. Vile vile waliomba wapewe sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea
shughuli na eneo la kujenga kituo cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha nje.
Ndugu Wananchi; Baada ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji gesi na mafuta
na kuelezwa mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara inahitaji kupanuliwa na
kujengwa upya. Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya Bandari walikuwepo na walinihakikishia
kuwa watafanya hivyo. Tayari eneo la bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68 hadi
2,693.68. Eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la kampuni ya Dangote
na makampuni ya gesi yaliyopo. Aidha, mchakato wa kupanua bandari iliyopo, kujenga
gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo ya Msanga Mkuu ipo katika hatua mbalimbali
za matayarisho na utekelezaji.
Ndugu Wananchi; Kwa upande
wa Mkoa wa Lindi mipango ya kupanua na kuijenga upya bandari ya Lindi imefikia hatua
nzuri. Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe
1 Desemba, 2012 nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi
ya tarehe 1 mpaka 5 Desemba, 2012. Hali kadhalika mipango ya kujenga bandari ya Kilwa
iko mbioni. Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya makampuni yaliyogundua gesi
baharini wameamua kujenga bandari na kituo cha kuchakata na kusarifisha gesi nje ya
mkoa huo kama ilivyo kwa Mtwara. Naambiwa wametambua maeneo matatu, kilichobakia
ni kuamua mojawapo ili ujenzi uanze.
Ndugu Wananchi; Nilipotoka
bandari ya Mtwara, siku ile nilitembelea Chuo cha VETA na kuzungumza na viongozi wa
VETA taifa na wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya kutoa
mafunzo mahsusi yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta. Nilisisitiza kwamba tuwapatie
vijana wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni ya gesi na yale yatakayokuwa
yanatoa huduma kwa makampuni hayo. Nilisema tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri
watu kutoka nje na hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu wala kulalamika.
Nafurahi
kwamba agizo langu hilo limefanyiwa kazi ipasavyo. Hivi sasa katika chuo cha VETA
Mtwara mafunzo hayo yanatolewa. Kampuni ya PetroBrass ya Brazil inaendesha mafunzo
ya sekta ya gesi kwa vijana 25 kutoka mkoani Mtwara. Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana
na Kampuni ya Gesi ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service Overseas ya Uingereza,
kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo Enhancing Employerbility Through Vocational
Training. Programu hii inalenga kutoa kozi zitakazowafanya wahitimu kuweza kuajiriwa
katika sekta ya gesi. Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.
Ndugu Wananchi; Chini
ya programu hii, walimu wa masomo yanayohusiana na gesi wanaongezewa ujuzi ili waweze
kufikia viwango vya kimataifa. Vile vile, Wizara ya Nishati na Madini imetoa upendeleo
maalum wa kudhamini wanafunzi 50 kutoka mkoa wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao tayari
wameshahitimu mafunzo ya msingi ya uunganishaji vyuma viwandani. Mchakato wa kuwapata
wanafunzi 50 kwa ajili ya mafunzo kama hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea. Nimeambiwa
mpaka wameshawapata vijana 25 bado 25. Hali kadhalika, Wizara ya Nishati
na Madini inadhamini wanafunzi 10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambako
kozi za mafuta na gesi zinatolewa. Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa kwa wanafunzi
wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa katika mafunzo haya. Wamepatikana
watatu. Wataalamu hawa na wengine wa fani mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa
kwa kiwango cha shahada ya kwanza na baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu ijitosheleze
kwa wataalamu wa sekta hii.
Kupanga Mji wa Mtwara Ndugu Wananchi;
Baada ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA, nilikaa na kuzungumza na viongozi
wa Serikali na Manispaa ya Mtwara. Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu
wa kuwa na mpango kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango
ambao utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa uchumi
wa gesi. Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda, biashara, makazi, mahoteli,
huduma za afya, elimu, mapumziko na burudani, viwanja vya michezo na kadhalika. Kazi
ya kutayarisha Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Makazi. Kwa upande wa uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa
makampuni 51 yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli, shughuli za
uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi. Wanachosubiri ni kutengewa maeneo ya kujenga,
waanze. Hivyo kukamilika mapema kwa Masterplan ya mji wa Mtwara kutasaidia kuongeza
kasi ya uwekezaji huu kufanyika. Viwanda hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa
vijana wa Mtwara na Watanzania kwa jumla. Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi
wa kiwanda cha saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla hata ya ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na mipango ya kutumia gesi
ya Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuzalisha mbolea na kutumika
katika kiwanda cha saruji. Kwa upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga mtambo
wa kuzalisha Megawati 300 kwa kushirikiana na mwekezaji binafsi. Bahati mbaya wakati
wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009 mwekezaji huyo akashindwa kupata mkopo,
hivyo mradi ukasimama kutekelezwa. Haukufa wala haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo
kama ambavyo imekuwa inapotoshwa kwa makusudi. Mradi huo bado upo, tena mpango wa
sasa ni kujenga Megawati 600 zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye gridi ya
taifa kupitia Songea.
NduguWananchi; Kwa upande wa kiwanda cha mbolea, wawekezaji
wengi wameshajitokeza tangu mwaka 2008 mpaka sasa. Mchakato umefanyika wa kuchambua
wawekezaji wenye sifa na kutambuliwa. Mambo mawili yamechelewesha utekelezaji kuanza.
Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya Artumas iliyokuwa mbia na Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (T.P.D.C) wakati ule, kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya
kuwauzia gesi. Wawekezaji walitaka bei ya gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya Artumas
na T.P.D.C. hawakuwa tayari kupunguza zaidi ya kiasi walichopunguza, ambacho wawekezaji
bado waliona hailipi kwa kuzalisha mbolea. Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha
yaliyoikumba kampuni ya Artumas katika kipindi hicho. Kufuatia machafuko ya masoko
ya fedha na mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas iliathirika
na kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine. Katika kipindi hicho ilichopitia
kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa kiwanda cha mbolea hayakuweza kupewa kipaumbele.
Mtazamo wa sasa wa wabia wapya na T.P.D.C. ni kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika
ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali imekubali rai yao hiyo na wanaendelea na matayarisho.
Ndugu
Wananchi; Kwa upande wa kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni
ya Dangote ucheleweshaji ulikuwa kwa sababu mbili. Kwanza, kampuni ya Dangote iliomba
eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na kupewa. Hoja yao ilikuwa kwamba eneo la ziada
walilokuwa wanaliomba ndilo lenye malighafi nyingi na bora kwa utengenezaji wa saruji.
Hivyo, waliamua kusubiri mpaka watakapopewa eneo hilo. Bahati mbaya eneo hilo
lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine na alikuwa na hati miliki nalo. Halmashauri
ya Mtwara iliomba Serikali eneo hilo litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote.
Serikali ilikubali. Hata hivyo, mchakato ulichukua muda na hata pale ulipokamilika
mwenye eneo aliupinga uamuzi wa Serikali Mahakamani. Kesi ilichukua muda kusikilizwa
na kumalizika. Bahati nzuri Serikali ikashinda na mara baada ya uamuzi wa Mahakama
ndipo kampuni ya Dangote ikamilikishwa eneo hilo. Kampuni nayo ilichukua muda
kuanza. Hivi sasa, timu yake ipo kwenye eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa.
Niliambiwa kuwa katika magari yaliyopigwa mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na
lile la mradi huu. Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote.
Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya kweli. Ni uzushi wa makusudi
wa watu wenye nia mbaya na Serikali. Huwezi kudai kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara
kwa hoja za uongo na kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu. Zilijengwa hisia kuwa gesi
yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatayotokana
na gesi hiyo. Na, wengine wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi
na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba Rais anapeleka gesi kwao.
Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo. Pili, ukweli ni kwamba pale Mtwara
kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kubaki.
Gesi itakayoletwa Dar es Salaam ni asilimia 16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa
miaka ishirini ijayo. Hivyo asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa
nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.
Kwa sababu hiyo, ndugu
zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa na wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji
ya sasa na ya miaka mingi ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na vile
vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha. Kwa upande wa uzalishaji
umeme hali kadhalika ipo gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi. Hivi sasa
tunacho kituo kinachozalisha umeme wa megawati 15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba,
Newala, Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote hivi
sasa.
Ndugu Wananchi;
Nayaeleza yote haya kuwathibitishia
wananchi wa Mtwara kuwa tunawathamini sana na kuwajali. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho
kuwapuuza na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya Kusini. Aidha, sitakuwa tayari kuwaruhusu
watu au mtu ye yote Serikalini kuwapuuza wananchi wa Mikoa ya Kusini au mkoa wo wote
hapa nchini. Hiyo haitakuwa sawa. Nilishasema siku za nyuma na napenda kurudia tena
leo kuwa kwangu mimi hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine. Ni kutokana na msimamo
wangu huo ndiyo maana tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali katika mikoa
iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa. Kazi ya ujenzi wa barabara za lami iliyofanyika
na inayoendelea kufanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na
Kagera inajieleza yenyewe. Mipango ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kufikia
hadhi ya kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa ni ushahidi
mwingine kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.
Ndugu Wananchi;
Haya niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa na kuelezwa kwa kina
na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika za Serikali na Mashirika ya Umma pale Mtwara
katika mkutano wa Waziri Mkuu na viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa na wazee
wa Mkoa wa Mtwara tarehe 29 Januari, 2013.
Ndugu Wananchi; Napenda kutumia
nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa kazi
kubwa na nzuri aliyoifanya kule Mtwara. Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake
vimesaidia sana kulivusha taifa katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi
yetu tangu Uhuru. Nawapongeza Mawaziri na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Idara za
Serikali kwa mchango wao muhimu walioutoa, uliosaidia kufafanua masuala ambayo yalikuwa
hayaeleweki vizuri. Kwa wao nawasisitiza na kuwakumbusha wajibu wao wa kuelimisha
jamii kuhusu shughuli wazifanyazo. Wakifanya hivyo mara kwa mara migongano haitakuwepo
na wapotoshaji hawatapata nafasi.
Ndugu Wananchi; Nitakuwa mwizi
wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya
dini, viongozi wa jamii, wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii, kwa muda
waliotumia kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake wakifafanua masuala
mbalimbali. Uvumilivu wao na uelewa wao ndivyo vilivyosaidia kurejesha hali kuwa
ya kawaida. Nawaomba nao sasa, wote kwa pamoja washirikiane na Serikali kuelimisha
umma kuhusu ukweli wa mambo.
Pia watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii
na kuwataka watu kuwa waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu. Wajiepushe
na maneno au vitendo vinavyofarakanisha, kuchonganisha na kupandikiza chuki dhidi
ya watu au Serikali. Waambieni kuwa ghasia hukimbiza wawekezaji kwani wakipata hofu
kuwa hali ya amani na usalama ni ya mashaka, watatoka kwenda kuwekeza kwingine. Vyema
iwe hapa hapa nchini, lakini wanaweza kwenda nchi nyingine na sisi kupoteza kabisa.
Ndugu
Wananchi; Nawapa pole wananchi wa Mtwara na Masasi kwa usumbufu walioupata
kutokana na ghasia zilizofanywa. Nawapa pole waliofiwa na kujeruhiwa. Nawapa pole
waliopoteza au kuharibiwa mali zao. Kwa kweli inasikitisha na kufadhaisha kuona watu
wanafanya vitendo vya kuua, kuchoma moto nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja
na , kuharibu na kuiba mali za watu. Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na haukubaliki.
Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza wajibu wao. Kwa waliohusika
iwe fundisho kwao na kwa wengineo kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wengine
siku zijazo. Sasa wameachwa pekee yao wakati wenzao wako huru na kufaidi maisha.
Ndugu
Wananchi; Hili sakata la bomba la gesi limefika mahali pazuri. Yaliyopita
si ndwele tugange yajayo.
Mungu Ibariki Afrika! Mungu Ibariki Tanzania! Asanteni
Sana kwa Kunisikiliza!