2013-02-04 09:24:21

Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani nchini Malawi


Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linamshukuru Mungu kwa kuliwezesha kupata miito mbali mbali ya maisha ya kitawa, linaendelea kusali kwamba, waamini wengi wataweza kutajirishwa na ushuhuda wa maisha na utume unaotolewa na watawa nchini humo. Itakumbukwa kwamba, Siku ya Watawa Duniani, inaadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe 2 Februari, Sanjari na Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni.
Ni Siku inayomwonesha Kristo Mwanga wa Mataifa, changamoto kwa watawa pia kuwa kweli ni mwanga wa mataifa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Kanisa Katoliki nchini Malawi linatambua na kuthamini mchango wa Watawa katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni ujumbe kutoka kwa Askofu Thomas Msusa, Mwenyekiti wa Tume ya Watawa, Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, katika Maadhimisho ya Siku ya kumi na saba ya Watawa Duniani.
Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, alisema Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili ni kielelezo makini cha watawa wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao; kwa njia ya Mashauri ya Kiinjili; yaani: Ufukara, Utii na Usafi kamili. Kuna umuhimu wa kuendelea kuadhimisha Siku ya Watawa Duniani kama kielelezo cha Kanisa kutambua na kuthamini maisha ya kitawa yanayojionesha kwa njia ya karama mbali mbali ambazo Roho Mtakatifu amelijalia Kanisa, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Hizi ni karama zinazojionesha kwa namna ya pekee katika huduma katika sekta ya: elimu, afya, maendeleo ya kijamii na majitoleo kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Watawa wamekuwa mstari wa mbele kushirikisha sala na imani yao kwa njia ya ushuhuda wa maisha, lakini zaidi pale wanapotangaza Injili na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ajili ya Watu wa Mungu.
Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani yawasaidie waamini kupata ufahamu mpana zaidi kuhusu Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume na jinsi ya kukabiliana na changamoto za maisha ya kiimani. Watawa wanapaswa kutambua kwamba, mchango wao ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Watawa wawe ni mfano wa kuigwa katika utamaduni wa Kusikiliza Neno la Mungu na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; chem chemi ya upendo na majitoleo makini. Wawe ni mashahidi wa uwepo wa Mungu kati ya watu wake.
Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2013 yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, changamoto ya kutambua kwamba, huu ni muda muafaka wa kufanya toba, wongofu wa ndani na kuendelea kuchuchumilia utakatifu wa maisha; kwa kujitahidi kumwilisha Mashauri ya Kiinjili katika hija ya maisha yao ya kila siku; wakiimarishwa kwa fadhila za imani, matumaini na mapendo kama njia ya kujishikamanisha na Mwenyezi Mungu.

Ndivyo Askofu Thomas Msusa anavyohitimisha ujumbe wake katika Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani, iliyoadhimishwa, hapo tarehe 2 Februari 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.