Patriaki Louis Raphael Sako wa Kwanza achaguliwa kuongoza Kanisa la Babiloni ya Wacaldei
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameridhia uchaguzi wa Patriaki Louis Raphael
Sako wa kwanza wa Kanisa la Babiloni ya Wacaldei, uliofanyika katika maadhimisho ya
Sinodi ya Kanisa hili iliyoitishwa na Baba Mtakatifu na kusimamiwa na Kardinali Leonardo
Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki. Kabla ya kuchaguliwa
kwake, Askofu mkuu Louis Sako, alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kerkut ya Wacaldei.
Patriaki mpya anachukua nafasi ya uongozi iliyoachwa wazi na Patriaki Emmanuel Delly
wa tatu. Na tangu sasa ataitwa Patriaki Louis Raphael Sako wa Kwanza.
Patriaki
Sako wa Kwanza alizaliwa kunako tarehe 4 Julai 1948 huko Zakho, Iraq. Baada ya masomo
na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 1 Juni
1974. Tangu wakati huo alitekeleza majukumu yake ya kichungaji hadi kunako mwaka 1979
alipotumwa Mjini Roma ili kuendelea na masomo ya juu na hatimaye, kujipatia Shahada
ya uzamivu katika Mafundisho ya Mababa wa Kanisa. Baadaye alijiendeleza pia katika
masomo ya historia na kujipatia Shahada ya pili ya Uzamivu katika Historia huko Paris,
Ufaransa.
Baada ya Masomo yake, kunako Mwaka 1986 alirudi mjini Mossul na kuteuliwa
kuwa Paroko wa Parokia ya Bikira Maria msaada wa daima. Kati ya Mwaka 1997 hadi mwaka
2002 alikuwa ni Gombera wa Seminari mjini Baghdad. Akarudi tena Mossul na kuendelea
na huduma yake ya Uparoko, hadi tarehe 27 Septemba 2003 alipoteuliwa kuwa ni Askofu
mkuu wa Jimbo kuu la Kerkuk na akawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu hapo tarehe 14 Septemba
2003.