Mshikamano wa Caritas na wananchi wanaoteseka kutokana na vita nchini Mali
Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Uswiss, Caritas limetoa kiasi cha Franc za Kiswiss
Laki moja, kama sehemu ya mchango wake kwa ajili ya kuwasaidia watu wasiokuwa na makazi
nchini Mali, wanaokimbia vita inayoendelea nchini humo kati ya Vikosi vya Wanajeshi
kutoka Ufaransa na Waasi wa Mali. Wahamiaji wengi ni wale wanaotoka Kaskazini mwa
Mali na kukimbilia Kati na Kusini; ambako kwa sasa kunaonekana kuwa na unafuu wa ulinzi
na usalama.
Taarifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 9,000 waliokimbilia
katika nchi jirani ilikutafuta hifadhi ya maisha yao na wanaendelea kuhudumiwa na
wananchi katika maeneo haya. Lakini, kutokana na wingi wa watu na ukosefu wa rasilimali
fedha, chakula na mablanketi, wahamiaji hawa wamejikuta wanakabiliana na hali ngumu
zaidi. Wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi kutokana na kinzani pamoja na migogoro
ya kijamii inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia.
Msaada uliotolewa na
Caritas unalenga kutoa walau lishe kwa watoto wanaokabiliwa na utapiamlo wa kutisha,
ambao umeongezeka kwa asilia sita pamoja na dawa za kudhibiti magonjwa ya milipuko.