Maisha ya watawa yawe ni Habari Njema inayomwilishwa na kutangazwa; maisha yanayong'ara
kama Neno la Ukweli
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku kuu ya kutolewa
Bwana Hekaluni inayoadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe 2 Februari, sanjari na Maadhimisho
ya Siku ya 17 ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2013 amepembua kwa ustadi mkubwa Simulizi
la Utoto wa Yesu kadiri ya Injili ya Mtakatifu Luka. Familia Takatifu ya Yesu Maria
na Yosefu ilikuwa ni maskini; watu wa kawaida kabisa lakini wachamungu na watu waliokuwa
tayari kutekeleza Sheria kadiri ya Torati.
Kutolewa kwa Bwana Hekaluni anasema
Baba Mtakatifu linakuwa ni tukio la pekee kabisa kwani, Mwana wa Mungu anaingia ili
kulitakatifuza Hekalu na Waamini wanaolitumia. Yesu ndiye Kuhani mkuu na Mwanakondoo
wa Mungu atakeyetolewa sadaka: kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, ili kuweka
Agano Jipya na la Milele kati ya Mungu na binadamu. Kristo ndiye Mkombozi wa ulimwengu
anayekuja kuwashirikisha wanadamu upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.
Ni utimilifu
wa unabii uliotolewa kwenye Maandiko Matakatifu, kama wanavyoshuhudia Mzee Simeoni
na Anna. Ndiye mwanga unaowaangazia watu wake Israeli. Ndiyo mwanga uliokuwa umebebwa
na Wakuu wa Mashirika katika Maadhimisho ya Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni.
Katika
Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu anawaalika Watawa kutambua kwamba, ni mahujaji wanaotembea
na Kanisa ili kuweza kuimarishwa katika imani, ili kujitoa kikamilifu kwa Mungu na
Kanisa. Anawashukuru watawa wa mashirika na karama mbali mbali ndani ya Kanisa kwa
uwepo na utume wao ndani ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla.
Maisha yao yawe
ni changamoto ya kuingia katika mlango wa Imani ambao daima uko wazi, ili kuweza kurutubisha
wito na mapendo yao kwa Kristo. Wajifunze ukimya wakati wa kuabudu, ili kuweza kuwashirikisha
wengine utii katika imani, ufukara katika mapendo na usafi kamili kwa ajili ya huduma
kwa Mungu na jirani.
Imani iwasaidie kutambua hekima inayojionesha katika udhaifu
pamoja na Fumbo la Msalaba, wakitambua kwamba, katika udhaifu wao wa kimwili, wanachangamotishwa
kumuiga Kristo ili waweze kufanana naye, daima wakijitahidi kuwa ni sauti ya wanyonge
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii inayotafuta kwa udi na uvumba: tija na
ufanisi.
Baba Mtakatifu anawaalika watawa kuuisha imani yao ili kuendeleza
hija ya maisha ya baadaye inayotafuta sura ya Kristo. Hali hii ijioneshe katika kila
hatua na wakati wa kufanya maamuzi mazito ya maisha. Watawa wajitahidi kujivika silaha
za mwanga, wakiwa makini na kuendelea kukesha, ili kwa njia ya huruma na neema yake,
waendelee kuwa ni waaminifu kwa Kristo mwenyewe.
Maisha yao kama Watawa yanawashirikisha
pia lile Fumbo la Msalaba kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ambaye moyo wake ulichomwa
kwa upendo wa Mungu. Mateso na magumu wanayokumbana nayo ni mwanga katika azma ya
uinjilishaji wa watu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika
mahubiri yake, anawataka watawa kuhakikisha kwamba, maisha yao yanakuwa ni Habari
Njema iliyomwilishwa na kutangazwa; maisha yanayong'ara kama Neno la Ukweli.