2013-02-02 09:49:31

Imani na upendo ni chanda na pete!


Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013, itakayoadhimishwa hapo tarehe 11 Februari 2013; Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013 pamoja na ujumbe wa Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya katika Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Ukoma Duniani; ni nyaraka zinazohitaji kufanyiwa tafakari ya kina kwani zinagusa: imani na upendo.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, iwe ni fursa makini ya kuweza kumwilisha Imani katika matendo, kwani fadhila hizi zinategemeana na kukamilishana katika hija ya maisha ya mwamini. Huu ndio uzuri wa ukweli wa maisha ya Mama Kanisa, unaolifanya liweze kuaminika na kuugusa undani wa maisha ya mtu unaojikita katika mwanga angavu na joto la upendo. Ni upendo ambao mwamini anajifunza kwa njia ya Imani kutoka kwa Mungu kwa kumwangalia Yesu Msalabani pamoja na kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Hii ni sehemu ya tahariri ya Padre Federico Lombardi, Mkurugeni mkuu wa Radio Vatican na msemaji mkuu wa Vatican kwa Juma hili. Watakatifu Bernadetha, Theresa wa Lisieux, Raoul Follerau, Padre Damiani, Mtakatifu Vinsenti wa Paulo na Mama Theresa wa Calcuta ni kati ya miamba ya imani na upendo waliojitahidi kumwilisha fadhila hizi kwa kujitoa bila ya kujibakiza, kwa wote waliokuwa wanateseka: kiroho na kimwili.

Waliwamegea utajiri uliokuwa umesheheni mioyoni mwao kuanzia wale wadogo hadi wale wa mwisho kabisa katika Jamii, wakisukumwa kutenda yote haya kwa Sheria ya Upendo. Kama anavyosema Mtakatifu Agustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa “Penda na tenda kile unachotaka” Upendo unavuka mipaka ya sheria na sheria zote anasema Padre Lombardi, zinapafanya rejea makini katika fadhila hii. Sheria hii inapaswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa.

Katika Kanisa wanyenyekevu wa moyo wanaonja upendo wa Mungu; wagonjwa wanatambua kwamba, ugonjwa wao pia ni kielelezo cha upendo ambao ni mkubwa zaidi wanaoweza kuutolea sadaka pamoja na Kristo.

Imani na Upendo, ni chanda na pete. Padre Federico Lombardi anahitimisha tahariri yake kwa kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujitaabisha kusoma tena nyaraka hizi, ili kuzipa uzito unaostahili!








All the contents on this site are copyrighted ©.