Wahamiaji kutoka Afrika wanaoishi Australia ni Familia ya Mungu inayowajibika barabara!
Ujumbe wa Maaskofu Katoliki kutoka Sudan ya Kusini, uliokuwa chini ya Askofu msaidizi
Santo Loku Pio, hivi karibuni, ulifanya hija ya mshikamano wa imani nchini Australia,
ili kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo waliohamishiwa nchini humo na sasa wanaendelea
na maisha yao kama waamini wa Kanisa Katoliki na raia wa Australia.
Hija hii
ni kielelezo cha mshikamano uliooneshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Australia,
kwa kuwaalika viongozi wa Kanisa kutoka Sudan ya Kusini, ili kwenda kuwaimarisha ndugu
zao katika imani na uwajibikaji, wakitekeleza wajibu na majukumu yao kwa weledi na
majitoleo makubwa.
Askofu msaidizi Santo anasema, amefurahia kuona na kusikia
kwamba, Wahamiaji hao ambao wengi wao ni kutoka Sudan ya Kusini, wanashiriki katika
maisha na utume wa Kanisa nchini Australia kama Makatekista, Mashemasi wa Kudumu na
kwamba, kuna baadhi ya Mapadre kutoka Barani Afrika wanaowahudumia ndugu zao katika
imani. Ili kutekeleza dhamana na wajibu huu, Kanisa Katoliki nchini Australia limewekeza
maradufu katika majiundo ya awali na endelevu na sasa wanachapa kazi barabara!
Baraza
la Maaskofu Katoliki Australia linasema kwamba, kuna Waamini wengi kutoka Barani Afrika
hasa zaidi kutoka katika nchi za DRC. Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya na Tanzania.
Kwa pamoja wanaunda Familia ya Mungu inayowajibika. Changamoto kwa waamini hawa ni
kuendelea kuwajibika kikamilifu, daima wakijitahidi kuwa ni raia wema, waaminifu na
wachapakazi; watu ambao wanafuata sheria na kanuni za wenyeji wao.