2013-02-01 07:57:50

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa


Tunaendelea na Neno la Mungu tafakari masomo Dominika, tayari tuko Dominika ya IV ya kipindi cha mwaka C, na Neno la Mungu latualika kutambua kuwa wale watakaojibidisha kutafuta uhuru na ustawi wa maisha ya watu watapata taabu na watambue hawatapata heshima hata siku moja na hasa nyumbani kwao. Jambo hili linaelekezwa kwa wale wanaoitwa kutoa ushuhuda wa upendo kwa mataifa. RealAudioMP3

Katika somo la kwanza tunasikia simulizi la wito wa Yeremia. Huyu alikuwa kijana mdogo wa miaka 20 hivi wakati anaitwa na Bwana. Kwa hakika alikuwa kijana mwema na mwenye akili. Matarajio yake yalikuwa ya kupata mchumba na baadaye kuoa! Lakini ghafla anaitwa na kuambiwa kabla ya kutungwa mimba yako nalikujua na kukuchagua, hivi nenda ukafanye kazi yangu. Mungu anaita tangu tumboni na anakabidhi kazi nzito ya imisionari ambayo ilimfanya Nabii Yeremia kupoteza hata marafiki. Maisha yake yalikuwa magumu kwa sababu ya unabii.

Kwa nini chuki dhidi ya Manabii? Ni kwa sababu wanaona ulimwengu kwa jicho la kimungu na hawawezi kukaa kimya kama mambo yanaenda kinyume na mpango wa Mungu!

Mpendwa mwana wa Mungu, tukirudi nyuma kidogo Nabii Yeremia anapoitwa, anasema mimi mdogo, sijui kusema! Toka hilò twajifunza visingizio vya mwanadamu vinavyojisimika katika kutegemea nguvu zetu wenyewe badala ya nguvu za Mungu. Tunaalikwa na maneno ya Bwana “hawatakushinda nipo pamoja nawe” daima kutoogopa kazi ya kimisionari.

Katika somo la II Mt Paulo anawafundisha Wakorinto akiwaonya juu ya mgawanyiko katika jumuiya yao unaotokana na majivuno, wakijivunia karama mbalimbali walizozipokea toka kwa Mungu. Anasema karama ni kwa ajili ya kujenga Jumuiya na si kwa ajili ya kubomoa au kukomaza mabega! Anaendelea pia kukazia somo la upendo, maana anaona katika jumuiya hiyo wapo wanaochanganya kati ya maraha ya dunia na upendo wa kimungu.

Anasema upendo hautafuti uzuri bali huunda uzuri. Mungu hakumpenda mwanadamu kwa sababu ni mwema bali alimpenda ili amfanye mwema. Upendo ni wa milele. Mpendwa angalieni mwelekeo wako kuhusu upendo, kama unalingana na tabia za upendo ambazo Mtakatifu Paulo anatufundisha hivi leo katika barua kwa Wakorinto.

Katika Injili tunapata mwendelezo wa Injili ya Dominika iliyopita. Bwana yuko katika utume wake na ghafla dharau kali inajipenyeza katikati ya watu na wanamwona Bwana mtu mjinga asiyejua kitu. Na dharau hii eti ni kwa sababu ni mwana wa seremala! Wanadai ahakikishe kuwa yeye ni Mwana wa Mungu kwa kufanya miujiza hapo nyumbani kwake! Na kwa sababu miujiza hulenga kukomaza imani hatafanya kwa sababu hawaamini kumbe itakuwa mazingaombwe! Kwa kisa hiki wanataka kumwangamiza, lakini anapita katikati yao! Oneni uovu huo wanamtoa nje Mwana wa Mungu! Mpendwa sisi nasi twafanya hilohilo pasipo mashaka! Tunaposahau misingi ya amani na mapendo katika nchi yetu.

Bwana anataka kuwafundisha watu hawa kuwa wokovu si kwa miujiza bali kuishi upendo kwa kutoa maisha yake, kuhubiri Neno la Mungu ndiyo shime yake. Maneno yake ndiyo hubadili maisha ya watu na kujenga jumuiya mpya na si miujiza ambayo waliisubiri. Wakati wetu huu wapo wengi wapenda miujiza yafaa kuwa makini. Angalia kama hata wewe unaomwelekeo huo!

Mpendwa wale watu waliomkazia macho kwa furaha Dominika iliyopita ndio haohao wanaomgeuka na kutaka kumwua, kuweni macho katika kuhubiri Neno la Mungu watu waweza kugeuka na kuwa mbogo, kumbe jiandae kwa nguvu ya neema za Mungu na upendo mkamilifu ili kuwashinda kwa upendo na msamaha kama Bwana alivyofanya.

Ninakukumbusha kuwa maisha yako yawe ni ya sala siku zote na si kusali wakati wa njaa, taabu, wakati wa mitihani nk. Mkristo ni Nabii wa mapendo na hivi wokovu ni kwa ajili ya wote, mmepewa bure toeni bure pasipo kudai malipo yasiyostahili.

Nikutakie heri na baraka tele katika Dominika hii na zile zijazo. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.