Siku ya Wagonjwa Duniani 2013: changamoto ya kuwa Wasamaria wema, kielelezo cha imani
tendaji
Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, kuanzia
mwaka 2013 litakuwa linachapisha vitini maalum kwa lugha mbali mbali, ili kuwawezesha
waamini na watu wenye mapenzi mema kuweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho
ya Siku ya Wagonjwa Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari,
sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes.
Vitini hivi
vitatolewa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yatakayomba ili yaweze pia kuchapisha
nakala kwa ajiliya Majimbo yao mintarafu ujumbe utakaokuwa umetolewa na Khalifa wa
Mtakatifu Petro kwa mwaka husika. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita kwamba, vitini hivi vitaweza kutumika kwa Mwaka mzima wa Liturujia ya Kanisa,
ili kuwawezesha waamini kukua na kukomaa katika imani, sala na tafakari ya kina kutoka
ndani ya Kanisa.
Vitini hivi vimegawanywa katika sehemu kuu tatu za Mwaka
wa Liturujia ya Kanisa: yaani: Kipindi cha Majilio, Noel ina Maadhimisho ya Siku ya
Wagonjwa Duniani inayofikia kilele chake kila mwaka tarehe 11 Februari kwa Maadhimisho
ya Siku kuu ya Bikira Maria wa Lourdes; Kwaresima pamoja na Kipindi cha Pasaka. Kutakuwa
na Njia ya Msalaba ili kuwasaidia wagonjwa na wadau mbali mbali kuweza kutafakari
kuhusu Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Ni maelekezo
yaliyotolewa na Mheshimiwa Padre Augusto Chendi, Katibu mwambata, Baraza la Kipapa
la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, kama sehemu ya maandalizi
ya Maadhimisho ya Siku ya 21 ya Wgonjwa Duniani inayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe
11 Februari.
Baba Mtakatifu anapenda pia kuonesha uwepo wake wa karibu katika
mahangaiko na mateso ya wagonjwa ndiyo maana amemtuma Askofu mkuu Zygmunt Zimowski
kumwakilisha katika maadhimisho haya katika madhabau ya Bikira Maria wa Altotting,
yaliyoko nchini Ujerumani. Lengo ni kuonesha moyo wa huruma na upendo kwa wagonjwa,
dhamana inayoendelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake.
Ili kuwawezesha
waamini kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatoa pia rehema kamili na za muda kwa waamini
watakaotimiza masharti yanayotolewa na Mama Kanisa, yaani kwa kupokea Sakramenti ya
Kitubio, Ekaristi Takatifu na Kusali kwa nia za Baba Mtakatifu. Rehema kamili na zile
za muda zinatolewa kati ya tarehe 7 hadi tarehe 11 Februari 2013.
Padre Chendi
anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa Maadhimisho
ya Siku ya 21 ya Wagonjwa Duniani anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kuwa ni Wasamaria wema kwa jirani zao, kama kielelezo cha imani tendaji.