2013-02-01 11:49:44

Mama Kanisa anapenda kuwekeza katika Majukwaa ya Vijana kwenye mitandao ili kuwajengea msingi wa imani na matumaini!


Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, Kanisa linapaswa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, "lina kula sahani moja" na vijana wa kizazi kipya, kwa kuwafuata kwenye maskani yao, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano unaopania mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya vijana wenyewe: kiroho na kimwili. Ni changamoto hii ambayo itafanyiwa kazi na Baraza la Kipapa la Utamaduni, linaloanza mkutano wake mkuu hapo tarehe 6 hadi 9 Februari, 2013 hapa mjini Vatican.

Anasema, Mtakatifu Yohane Bosco ni kiongozi wa Kanisa aliyefaulu kuwafahamu, kuwapenda na kuwasaidia vijana katika hija ya maisha yao: kiroho na kimwili. Hata vijana wa kizazi kipya wanazo changamoto wanazopaswa kuzifanyia kazi, lakini pia wanabeba ndani mwao utajiri mkubwa wanaopaswa kuwashirikisha wengine, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Vijana wanapaswa kuwa makini ili wasitumiwe na baadhi ya watu wanaotaka kuwatumbukiza katika maafa yanayojitokeza katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Wasikatishwe tamaa na ukosefu wa fursa za ajira, janga ambalo ni matunda ya myumbo wa uchumi kimataifa. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kujifunza lugha ya vijana wa kizazi kipya, ili liwajengee jukwaa makini la kuweza kuwasiliana na Kanisa pasi ya woga na kwa ufanisi mkubwa.

Kardinali Ravasi anawataka viongozi wa Kanisa na Jamii kwa ujumla kuwa na imani na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kutambua na kuthamini mchango wao katika maisha na ustawi wa Jamii inayowazunguka, hasa katika zile kazi za kujitolea, ambazo mara nyingi vijana wameonesha kuwa katika mstari wa mbele. Vijana wanapaswa kujengewa uwezo na kupewa dhamana ya kushika madaraka pasi na kuwa na kigugumizi cha utendaji na uwajibikaji wao, kwani wakithaminiwa kwa hakika wanaweza kutenda maajabu!

Mama Kanisa anao wajibu mkubwa, kuhakikisha kwamba, vijana wanashirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa kuanzia katika: Familia, Jumuiya Ndogo ndogo, Vyama vya Kitume, Parokia na Majimboni. Hii ndiyo changamoto kubwa iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican, yapata miaka 50 iliyopita; daima Kanisa lijitahidi kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa wahusika. Siri ya mafanikio haya ni toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kuiamini Injili.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Mama Kanisa anapenda zaidi na zaidi kuangalia imani na matumaini ya vijana wa kizazi kipya, licha ya taabu, magumu na mahangaiko wanayokabiliana nayo katika ujana wao, kwani kwa kawaida ujana ni mali! Ni kipindi cha mtu kuwa na ndoto za kufikirika, lakini pia ni wakati ambapo kijana anaweza kujikuta akiteteleka na kutembea katika giza na utupu wa maisha, kama inavyojionesha katika athari za myumbo wa uchumi kimataifa; kinzani na migogoro ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Vijana wajengewe matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.