Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa
Bwana Hekaluni, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari ya kila mwaka,
anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro,
mjini Vatican kwa ajili ya Watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Ibada
hii itafanyika majira ya jioni.
Baba Mtakatifu katika Waraka wake kuhusu Mwaka
wa Imani, "Porta Fidei" Mlango wa Imani anabainisha kwamba, kwa njia ya imani, kuna
watu ambao wamewekwa wakfu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; wakaacha yote ili kuanza
kujikita katika mashauri ya Kiinjili, yaani: utii, ufukara na usafi kamili. Hawa ni
kielelezo makini cha wale wanaomsubiri Kristo ambaye, kamwe hatachelewa kurudi.
Siku
ya Watawa Duniani ilianzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, yapata miaka kumi
na saba iliyopita, ili kutoa nafasi kwa Mama Kanisa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya
maisha ya kitawa, watu ambao ni mfano na kielelezo cha kuigwa. Ni nafasi pia ya kuombea
miito mbali mbali ndani ya Kanisa.