Vurugu za kugombania maliasili Tanzania na athari zake!
Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali ya Tanzania italipa uzito wa kipekee suala
la uendelezaji wa Ukanda wa Kiuchumi wa Mtwara (Mtwara Corridor) kama ilivyo kwa Ukanda
wa Kilimo wa Nyanda za Juu Kusini Tanzania (SAGCOT). Serikali itachukua hatua hiyo
ili kuiendeleza kiuchumi mikoa ya kusini ambayo ni Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Ametoa
kauli hiyo Jumanne, Januari 30, 2013 mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi
wa habari ili kutoa ufafanuzi juu ya suala alilokwenda kufuatilia mkoani Mtwara kufuatia
vurugu zilizozuka hivi karibuni kuhusiana na suala la uchimbaji gesi mkoani humo.
Mbali na hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha Wizara ambazo zinawajibika
kutoa maelezo kuhusu uwekezaji na uendelezwaji wa miradi mkoani Mtwara zinaweka ratiba
maalum ya kwenda huko na kutoa maelezo ya kina kwa wananchi.
Alitumi fursa
hiyo kuwasihi wakazi wa mkoa huo kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaimarishwa kama
kweli wanataka mkoa huo uendelezwe. “Ninawasihi wakazi wa Mtwara waimarishe amani
na utulivu sababu fursa walizonazo ni kubwa sana. Ni vizuri viongozi na wananchi wa
mkoa huo wakajipanga vizuri ili waangalie namna watakavyonufaika na uwekezaji huo,”
alisema.
Akifafanua kuhusu mgogoro uliosababisha vurugu hizo, Waziri alisema
katika muda wa siku mbili alizokuwa Mtwara aliweza kukutana na vikundi tisa vilivyojumuisha
viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, madiwani, wafanyabiashara na vyombo
vya dola. Alisema baada ya kusikiliza pande zote, Waziri Mkuu aliwaita mawaziri wa
Elimu, Uchukuzi, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Viwanda na Biashara na Kaimu Mkurugenzi
wa TIC ili watoe ufafanuzi kwenye kikao cha majumuisho ambacho kilifanyika Jumanne,
Januari 29, 2013 mjini Mtwara.
“Ni bahati mbaya hali ilikuwa hivyo. Ni jambo
ambalo lisingetakiwa kufika hapo. Ni bahati mbaya kwamba elimu kuhusu uwekezaji mkoani
Mtwara haikuwa imefika kwa wananchi walio wengi, ni wananchi wachache waliofikiwa
wakati wa kutoa taarifa. Wabunge walijua jambo hili na walikuwa na wajibu wa kuwaelimisha
wananchi…,” alisema.
Waziri Mkuu alisema hoja kuu iliyotolewa na wakazi hao
ni kwamba walikuwa hawapingi gesi kwenda Dar es Salaam isipokuwa walikuwa wakitaka
kijengwe kiwanda cha kusafisha gesi pale Mtwara ili mabaki yanayotokana na usafishaji
huo yatumike palepale mkoani kutengenezea bidhaa nyingine kama vile mbolea na vifaa
vya plastiki.
Akielezea kuhusu hasara zilizosababishwa na vurugu hizo, Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi alisema nyumba, ofisi na magari vilichomwa
moto katika sakata hilo lililohusisha wilaya za Mtwara na Masasi Januari 25 na 26
mwaka huu. Alibainisha kwamba kwa wilaya ya Masasi pekee gharama za kurekebisha uharibifu
huo zinafikia sh. bilioni 1.5/-. Hata hivyo, alisema gharama halisi za uharibifu uliotokea
kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara pamoja na Manispaa ya Mtwara hazikuweza kupatikana
kwa haraka.