2013-01-31 09:07:38

Ukata na athari za mafuriko zinavyo vuruga huduma za Kijamii nchini Malawi


Mheshimiwa Padre Piergiorgio Gamba ambaye kwa miaka mingi amekuwa mstari wa mbele katika mapambano na huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi nchini Malawi anasema kwamba, fedha za kununulia dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa Ukimwi nchini Malawi zimepunguzwa kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba, wagonjwa wengi wameanza kukata tama na kwamba, juhudi zilizokuwa zinafanywa na Mashirika haya pengine sasa zikagonga mwamba na idadi ya waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi wakaongezeka.

Hali hii inatishia amani kwani wagonjwa wengi waliokuwa wanatumia dawa za kurefusha maisha, wanaweza kufariki dunia, kwani wengi wao wanakabiliwa na ukata ambao kwa sasa unachangiwa pia na athari za mafuriko yaliyoikumba Malawi kwa siku za hivi karibuni. Kama hali hii haitapatiwa ufumbuzi wa kudumu, wastani wa umri wa wananchi wa Malawi kuishi utaweza kushuka chini ya miaka arobaini. Kwa sasa watu wengi hawana makazi maalum baada ya makazi yao kusombwa na mafuriko.

Ukata pia unalikumba Kanisa ambalo linawezeshwa na waamini ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya uchumi, kiasi kwamba, huduma katika shughuli za kichungaji, elimu na afya zimeanza kuathirika kwa sasa. Umaskini ni kati ya changamoto zinazofanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, lililoanza mkutano wake hapo tarehe 28 Januari na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe Mosi Februari 2013.

Maaskofu pia wanajadili namna ya kutekeleza Maazimio ya Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, Mwaka wa Imani pamoja na maandalizi ya Mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, unaotarajiwa kufanyika nchini Malawi, hapo mwaka 2014.
All the contents on this site are copyrighted ©.