2013-01-31 15:34:53

Tamko la Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu Gesi, Mtwara


TAARIFA KUHUSU ZIARA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB.) WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BUNGENI; KUHUSU ZIARA MAALUM ALIYOIFANYA MKOANI MTWARA TAREHE 27 - 29 JANUARI 2013 KUFUATIA MATUKIO YA UVUNJIFU WA AMANI – ILIYOTOLEWA TAREHE 31 JANUARI, 2013

(Imetolewa chini ya Kanuni ya 38(4) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge)

  UTANGULIZI


Mheshimiwa Spika,
Hali ya ulinzi na Usalama Mkoani Mtwara ilikuwa ya utulivu kwa kipindi chote hadi tarehe 27 Desemba 2012 yalipofanyika maandamano ya Vyama mbalimbali vya Siasa na Wafuasi wao na baadhi ya Wakazi wa Mji wa Mtwara wakipinga Mpango wa Serikali wa kusafirisha gesi asilia kwa bomba kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Baada ya maandamano hayo, hali ya amani na utulivu katika Wilaya ya Mtwara na baadaye katika Wilaya ya Masasi ilianza kutoweka kwa kutokea matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani.

Hali ya Vurugu Mkoani Mtwara ilifikia kilele tarehe 25 na 26 Januari 2013 Mkoani Mtwara ambapo kulijitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani viliofanywa na vikundi vya vijana kwa lengo la kuharibu majengo ya Serikali, nyumba za Watu binafsi, nyumba za Viongozi wa Kisiasa, kuchoma moto na kuharibu magari ya Serikali na ya Watu binafsi; na miundombinu mingine ya Umma.

Tarehe 25 Januari 2013 Mjini Mtwara, kulitokea vurugu ambapo matukio kadhaa yalifanywa yakiwemo nyumba ya Diwani wa Kata ya Chikongola iliharibiwa kwa kupigwa mawe, nyumba ya Mhe. Hawa Ghasia inayoendelea kujengwa iliharibiwa kwa kupigwa mawe vioo vya madirisha pamoja na kuunguza sehemu ya jengo hilo, huko Magomeni, jengo la Ofisi ya Kata ya Ufukoni lilichomwa moto na nyaraka mbalimbali kuunguzwa, Mahakama ya Mwanzo ya Mjini Mtwara ilichomwa moto na kuteketeza nyaraka mbalimbali, kuchomwa kwa nyumba ya askari mmoja katika eneo la Sabasaba, kuvunjwa kwa duka la Diwani wa Kata ya Ufukoni na kuibiwa mali mbalimbali, kushambiliwa na kuibiwa vitu mbalimbali katika grocery ya Askari mmoja na Askari mmoja kujeruhiwa kwa kupigwa jiwe sehemu za kichwani; ambapo hali yake kwa sasa inaendelea vizuri.

Vurugu hizo ziliendelea tarehe 26 Januari 2013 katika Wilaya ya Masasi ambapo kulifanyika uharibifu mkubwa wa mali za Serikali, Viongozi na Raia. Vurugu hizo ni pamoja na kuchomwa kwa nyumba za Waheshimiwa Wabunge Mama Anna Abdallah na Mhe. Mariam Kasembe, kuunguzwa na kuteketeza ofisi za manunuzi Halmashauri ya Masasi, kuteketeza kwa moto ofisi ya elimu ya msingi na nyaraka zote, kuteketeza ofisi ya ukaguzi wa shule na TSD na nyaraka zote, kuunguzwa kwa ofisi ya Maliasili na nyaraka zote, kuharibiwa kwa baadhi ya Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, kuchomwa moto na kuteketea kabisa kwa magari kumi na moja (11) yaliyokuwa yameegeshwa katika yadi ya Halmashauri yakiwemo ya Serikali sita na ya watu binafsi matano. Kati ya magari ya Serikali yaliyochomwa yapo magari mawili ya wagonjwa (moja likiwa jipya kabisa). Uharibifu huo pia ulihusisha kuchomwa moto kwa pikipiki nne na baiskeli moja za Watu binafsi, pamoja na kuharibiwa kwa vifaa mbalimbali vya ofisi za Halmashauri. Vilevile, kuvunjwa kwa geti kuu la kuingilia Halmashauri, kuondolewa kwa uzio wa mabati katika jengo linalojengwa na Halmashauri, kuunguzwa kwa strong room ya Idara ya Maliasili na kuteketea kwa bunduki moja na kuunguzwa kwa shehena ya mbao zilizokuwa zimekamatwa na Halmashauri.

Vurugu hizo vilevile zilisababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 15 kutokana na mapambano kati ya Raia (Vijana) na Polisi. Aidha, Polisi mmoja alipigwa mapanga na kujeruhiwa vibaya ambapo kwa sasa amepelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwapa pole wale wote waliopateza Ndugu, Jamaa na Marafiki zao katika vurugu hizo. Aidha, nawapa pole waliopoteza mali na Majeruhi wote na kuwatakia warudi kwenye hali zao za kawaida.

Mheshimiwa Spika,
Kama utakavyoona, kiwango cha vurugu na uharibifu wa mali za Serikali na Raia kilikuwa ni kikubwa. Kufuatia hali hiyo, tarehe 27 Januari 2013, nililazimika kukatisha safari yangu ya kuja Bungeni Dodoma na kwenda Mkoani Mtwara. Lengo la Ziara yangu hiyo maalum ilikuwa ni pamoja na:

  Kujionea hali Halisi ya Ulinzi na Usalama Mkoani Mtwara;


  Kupata taarifa rasmi za matukio mbalimbali yaliyotokea katika siku za hivi karibuni Mkoani Mtwara kutoka Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya, na hatua zilizochukuliwa kukabiliana na hali hiyo;


  Kukutana na Wadau mbalimbali Mkoani Mtwara ili kusikia kutoka kwao nini hasa kiini cha vurugu hizo, na kuona namna ya kurejesha hali ya amani na utulivu Mkoani; na


  Mwisho ni kusikia maoni yao kuhusu suala zima la Gesi Mkoani Mtwara.

Mheshimiwa Spika,
Katika Ziara yangu Mkoani Mtwara niliweza kukutana na Makundi mbalimbali ya watu kusikia kutoka kwao sababu za kuzungumzia masuala ya usalama Mkoani humo na kupata maoni yao hususan katika suala zima la Gesi. Makundi niliyokutana nayo ni pamoja na:

  Viongozi wa Vyama vya Siasa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Wanaharakati;


  Viongozi wa Madhehebu ya Dini ya Kiislamu na Kikristo,


  Wafanyabiashara na Wakuu wa Taasisi mbalimbali zikiwemo Taasisi za Fedha wa Manispaa ya Mtwara,


  Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa; na


  Wajumbe wa Kamati za Siasa za Chama Tawala za Wilaya na Mkoa.
2.0 HOJA KUU ZILIZOJITOKEZA

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kuzungumza na Makundi hayo, niliweza kupata hoja na mapendekezo yao, mengi yakijielekeza katika suala zima la gesi na maendeleo ya Mkoa wa Mtwara. Hoja hizo kwa ujumla wake ni hizi zifuatazo:

  Kwamba, kimsingi Wananchi wa Mtwara hawana tatizo na gesi kupelekwa Dar es Salaam, bali wanachotaka ni kuona Mtambo wa kusafisha Gesi Asilia unajengwa Mtwara na kisha gesi hiyo ndiyo ipelekwe Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi mengine yakiwamo ya kufua umeme, kuuzwa ndani na nje ya Nchi kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya viwandani, nyumbani, n.k. Lengo la kutaka mpango huo ni pamoja na kuwa, kuwepo kwa Mtambo huo Mkoani Mtwara, utachochea maendeleo ya Mkoa huo na kuzalisha ajira kwa Wazawa wa Mtwara. Aidha, kuwa na uhakika wa Wawekezaji wengi kuanzisha viwanda Mkoani Mtwara kutokana na uhakika wa upatikanaji wa Nishati ya Umeme, jambo litakalosaidia ajira kwa vijana na upatikanaji wa bidhaa kwa bei nafuu kwa Wananchi wa Mtwara;


  Sambamba na suala hili la gesi, wametaka kujua lini Sera ya Gesi na Sheria ya Gesi vitakamilika tayari kwa matumizi ili wawe na uhakika wa kunufaika na rasilimali ya Gesi;


  Walieleza kuwa, Wana Mtwara wanakabiliwa na matatizo mengi ya msingi yakiwemo ya miundombinu ikiwemo kutelekezwa kwa Bandari ya Mtwara na kutokukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Mtwara - Dar es Salaam kipande cha (Ndundu-Somanga) ambao umechukua muda mrefu. Wameeleza kuwa, masuala haya yamezidi kufanya Maendeleo ya Wananchi wa Mtwara kuwa chini kiuchumi.


  Wananchi wa Mtwara pia walieleza kuwa, kutokana na kuvumbuliwa kwa gesi Mkoani humo, Serikali iliwaeleza kuwa, Wawekezaji wengi wameonyesha nia ya kujenga viwanda Mkoani hapo, kama vile kiwanda cha saruji, mbolea n.k. Hata hivyo, hofu yao ni kuwa viwanda hivyo bado havijajengwa. Hivyo, wangependa kujua hatma ya suala hili.


  Wananchi wa Mtwara pia wameeleza kuwa na tatizo kubwa la Viongozi wao wa Kisiasa Mkoani kuwa na mpasuko na kutokuelewana. Suala ambalo limewasababishia kutokuwa na maelewano na umoja wa Kimkoa na kupanga maendeleo yao kwa faida ya Wananchi wa Mkoa huo. Wameeleza kuwa, katika mpasuko huo, suala zima la maendeleo limetawaliwa na ubinafsi na hivyo kuwafanya warudi nyuma kimaendeleo.


  Wananchi wa Mtwara wanalalamikia Uongozi wa Mkoa kwa kutokuwasikiliza na kuwapokea pale walipojaribu kupeleka maoni yao kwa Mkuu wa Mkoa kupitia maandamano ya tarehe 27 Desemba 2012 kuhusu suala zima la gesi ya Mtwara kupelekwa nje ya Mkoa. Aidha, walieleza kupewa matamshi ya kuwadharau na kuwafedhehesha. Suala hili pia lilichangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha mahusiano ya Wananchi na Uongozi wao katika kupanga na kujadiliana masuala mbalimbali na hivyo kuwarudisha nyuma kimaendeleo.


  MAELEZO YA SERIKALI KUHUSU HOJA HIZO

Mheshimiwa Spika,
Hoja zilizotolewa na Wananchi wa Mtwara ni za muhimu. Nyingi kati ya hizo zinahitaji kutolewa maelezo ya jinsi gani zimeshughulikiwa na kutoa ufafanuzi pale ambapo panahitaji uelewa zaidi. Hivyo, naomba nichukue fursa hii kwa ufupi kuelezea masuala machache kuhusiana na hoja zilizotolewa na Wananchi wa Mtwara.

  MAELEZO KUHUSU UJENZI WA MTAMBO WA KUSAFISHIA GESI NA BOMBA LA GESI

Mheshimiwa Spika,
Ufahamu mdogo wa Mradi mzima wa Mtambo wa kusafishia gesi na ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaa ndio ulioleta hisia tofauti na hivyo kuchochewa na kusababisha vurugu zilizokuwa zimetokea Mkoani Mtwara. Ukweli wa Mradi huu kwa kiasi kikubwa umepotoshwa ama kwa kujua au kwa kutokujua.

Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka kuwa, kufuatia tatizo la umeme lililoikumba Nchi yetu katika kipindi cha mwaka 2011/2012 kutokana na ukame uliotokea na kukausha mabwawa yetu ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yanayotegemewa katika kufua umeme, katika kutafuta suluhu ya kupata umeme wa uhakika, ilionekana kuwa, njia nzuri na yenye uhakika ni kufua umeme kutokana na gesi Asilia.

Kimsingi, Gesi Asilia iliyogunduliwa hapa Nchini ni takribani Futi za Ujazo Trilioni 35. Ingawa tuna gesi kiasi hicho, kiasi kilichoendelezwa ni futi za ujazo Trilioni 1 tu. Kwa mantiki hiyo tunaweza kuona kuwa kiasi cha gesi kinachotumika ni kidogo sana ukilinganisha na kiwango cha Futi za Ujazo Trilioni 35 zilizogunduliwa.

Bomba la gesi asili linalojengwa litasafirisha gesi nyingi zaidi ambayo itawezesha mitambo mipya itakayojengwa Kinyerezi (Dar es Salaam) kufua umeme wa zaidi ya MegaWati 990.

Kwa kutumia Wataalam, Serikali ilifanya upembuzi yakinifu na kubaini kuwa, ni vyema gesi ikasafirishwa kwa njia ya Bomba hadi Dar es Salaam, kwani itakuwa na faida nyingi kuliko kufua umeme Mtwara na kusafirisha kwa Gridi. Walipokokotoa usafirishaji wa umeme ulionekana kuwa utahitaji “Line” zaidi ya moja, hivyo utakuwa ghali zaidi na pia usafirishaji wa umeme kwa kutumia nyaya na nguzo zake, kutasababisha upotevu mkubwa wa umeme njiani.

Katika Mpango mzima wa ujenzi wa Mtambo wa kusafishia gesi na bomba la kusafirishia gesi ni kwamba, tangu awali Serikali ina mpango wa kujenga Mtambo wa kusafishia gesi palepaleMkoani Mtwara eneo la Madimba, ambapo Gesi italetwa mpaka hapo kutoka kina kirefu cha Bahari na kusafishwa / kuchujwa na kisha kiasi cha gesi kitabaki Mkoani Mtwara kwa ajili ya matumizi ya viwanda, majumbani n.k. na nyingine kusafirishwa kwa bomba kwenda Dar es Salaam. Faida ya kusafirisha Gesi kwa bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni kama ifuatavyo:

  Bomba litawezesha kusambaza Gesi katika maeneo yote linapopitia kwa wateja wasio wa umeme. Mtwara - Lindi - Somangafungu na Mkuranga- Kinyerezi.


  Gesi hiyo hiyo itahudumia Viwanda (37) ambavyo vipo tayari Dar es Salaam; na


  Gesi hiyo pia itatumika kwa matumizi mbalimbali kama vile ya majumbani, kwenye magari, na kuuzwa nje ya Nchi kama bidhaa mojawapo itakayokuza Pato la Taifa.


Mheshimiwa Spika,
Kutokana na maelezo hayo, taarifa za kuwa Mtambo wa kuchakata / kusafisha Gesi asilia kuwa hautajengwa Mkoani Mtwara ni potofu kwani Gesi ni lazima isafishwe kabla ya kusafirishwa na Mtambo huo tayari upo katika Mradi mzima ukijumuisha ujenzi wa Bomba la Gesi ambao umekadiriwa kuchukua muda wa miezi 18.

Hoja kubwa inayojionyesha hapa ni kuwa Wananchi hawakupewa elimu ya kutosha kuhusu Mradi huu ikiwa ni pamoja na kueleweshwa mpango mzima wa Gesi ikiwa ni pamoja na kujua fursa zilizopo na jinsi Wananchi watakavyohusika nazo; Kama vile katika ajira, biashara, elimu, n.k. Hali hii ndiyo imetoa nafasi kwa watu mbalimbali kutafsiri isivyo na kupotosha ukweli wa suala hili. Kutokana na hali hiyo, suala hili limeibua hisia na hasira kwa Wananchi ambao kimsingi hawakuwa na ufahamu sahihi wa mpango nzima.

Ninaelewa kuwa, awali Uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) walitoa elimu kwa kundi la Watu wachache, wakiwemo wale walioathirika na upitishwaji wa Bomba la Gesi Asilia na wale walio karibu na Bomba hilo ili wawe walinzi shirikishi pamoja na Viongozi wa Siasa, Mashirika yasiyo ya Serikali, Wanaharakati n.k kwa lengo la kundi hilo kwenda kutoa elimu kwa Umma. Hata hivyo, imeelezwa kuwa, wale wachache waliopata elimu hiyo wamekuwa wakipotosha ukweli wa Mradi huo kwa maslahi yao binafsi kwa kutilia maanani kuwa Wananchi wengi hawana uelewa sahihi juu ya suala hili.

Ninapenda kuwajulisha kuwa, baada ya kuzungumza na makundi mbalimbali kama nilivyoyataja na kuwaelewesha Mpango huumzuri wa Serikali, walielewa na kukiri kuwa walikuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu Mradi huu.

  SUALA LA SERA NA SHERIA YA GESI

Mheshimiwa Spika,
Ili kufanikisha matumizi endelevu ya gesi asilia, Serikali imeazimia kukamilisha mapema iwezekanavyo Sera ya Gesi Asilia na Sheria ya Gesi. Sera ya Gesi Asilia ipo katika hatua za kukamilika kwake baada ya Serikali kufanya mikutano Nchi nzima na kukusanya maoni ya Wadau mbalimbali kwa lengo la kukamilisha Sera hiyo. Baadhi ya Wadau walioshirikishwa ni pamoja na Wananchi wa kawaida katika Mikoa ya Tanzania hususan ile inayotoka katika Ukanda wa gesi ikiwemo Mtwara, Lindi na Pwani; Makampuni ya wachimba Gesi na Mafuta yaliyopo Nchini, Wanataaluma kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Wataalam mbalimbali wa Gesi, Makundi ya Kijamii n.k.

Sambamba na Sera ya Gesi asilia, Serikali imeshaanza kuandaa rasimu ya Sheria ya Gesi ambapo ikikamilika, itapitishwa katika ngazi stahiki na hatimaye kuwasilishwa katika Bunge lako Tukufu.

  SUALA LA MIUNDOMBINU YA MAENDELEO MKOANI MTWARA IKIWAMO BANDARI

Mheshimiwa Spika,
Ili kutengeneza mazingira mazuri ya biashara ya gesi asilia na mafuta kwa Makampuni ya huduma, malighafi na vitendea kazi, Serikali imetenga eneo maalumu Mkoani Mtwara, ambalo litawekewa miundombinu ya msingi ili kuweka vivutio mbalimbali kwa Makampuni hayo. Eneo hilo litapewa hadhi ya Ukanda Huru wa Bandari (Freeport Zone).

Eneo hilo litavutia Makampuni mbalimbali kuja kuwekeza kwa nia ya kuhudumia na kufanya biashara na Makampuni yenye visima vya gesi nchi kavu na kina kirefu baharini. Makampuni makubwa duniani yameonesha nia ya kuja kuwekeza ili yafanye biashara na makampuni yaliyoko sasa kusini mwa Tanzania na hata nchi jirani ya Msumbiji badala ya kupata huduma hizo kutoka Qatar ambako ni mbali. Kuwepo kwa maendeleo hayo Mkoani Mtwara, kutaharakisha maendeleo ya kiuchumi na kubadilisha kabisa hali ya uchumi ya Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Kuhusu ujenzi wa Barabara kipande cha Ndundu - Somanga, kati ya Kilometa 62 zilizokuwa zimebakia kujengwa, Serikali inakamilisha ujenzi huo ambapo kwa sasa zimebaki Kilomita 20 tu. Ujenzi huu ulichelewa kukamilika kutokana na matatizo yaliyokuwa yamejitokeza katika Kampuni ya Karafi inayojenga barabara hiyo baada ya Mmiliki wake kufariki. Kwa sasa Kampuni hiyo inaendelea na ujenzi wake na Serikali inaahidi kuisimamia ili ujenzi huo ukamilike ndani ya mwaka huu.

  UWEKEZAJI WA VIWANDA MKOANI MTWARA


Mheshimiwa Spika,
Baada ya neema hii ya gesi Mkoani Mtwara, Wakazi wa Mtwara mbali ya kufaidika kwa gesi asilia ambayo itakuwa ni chanzo cha uhakika cha umeme na matumizi ya gesi moja kwa moja watafaidika pia na kuwepo kwa Wawekezaji wengi walioonyesha nia ya kuwekeza Mkoani Mtwara kutokana na fursa hii. Mpaka sasa kuna Makampuni yapatayo 51 ambayo yameonyesha nia ya uwekezaji katika viwanda vya Saruji, Mbolea, Sekta ya Usafirishaji, Kilimo na Usindikaji, na kuwekeza katika Utalii. Aidha, mabaki ya gesi baada ya kusafishwa ni malighafi muhimu kwa baadhi ya viwanda vikiwemo vya mbolea, kemikali petrol, bidhaa za plastiki, n.k.

Kutokana na kujengwa kwa viwanda hivyo na uwekezaji unaotarajiwa Mkoani Mtwara, tatizo la ajira Mkoani humo litapungua kwa kiasi kikubwa. Nimeelezwa kuwa, moja ya viwanda vikubwa vitakavyojengwa, kitahitaji Watumishi wa kawaida takriban 50,000 na Wataalam 2,000. Hakika huu utakuwa ni ukombozi mkubwa wa ajira kwa Wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla. Kampuni ya Dangote inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha Saruji Mkoani Mtwara ambacho kimeelezwa kuwa moja ya Viwanda vikubwa vya Saruji Barani Afrika, nacho kitatoa ajira nyingi na za uhakika kwa Wana Mtwara. Niseme tu kuwa, Wananchi wa Mtwara wawe na subira katika mipango hii kwani ni ya uhakika.

Mheshimiwa Spika,
Ili kuhakikisha kuwa Wananchi wetu wakiwemo wa Mtwara na hususan Vijana wananufaika na ajira za maana katika miradi ya gesi na viwanda vitokananvyo na fursa za gesi, Serikali imejipanga katika kuelimisha watu wetu kama ifuatavyo:  SUALA LA KUTOKUELEWANA KWA WANANCHI NA UONGOZI WA MKOA WA MTWARA

Baada ya kusikia malalamiko kutoka kwa Wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuhusiana na mahusiano mabaya ya Wananchi na Mkuu wa Mkoa baada ya kusemekana kuwadharau na kuwakejeli Wananchi wa Mtwara, tatizo hili kwa sasa nina uhakika litakuwa limekwisha. Juzi kabla ya kuhitimisha Ziara yangu Mkoani Mtwara na kabla ya kufanya majumuishao, Mkuu wa Mkoa Mhe. Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia alionyesha uungwana wake kwa kupitia hadhara iliyokuwepo kwa kuomba radhi Wananchi wa Mtwara kwa matatizo yaliyojitokeza na kuwaomba waendelee na ushirikiano wao kwa lengo la kuujenga Mkoa wa Mtwara ambao una mategemeo mengi. Napenda kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kuonyesha uungwana wake na ukomavu wake. Kiongozi huyu ni Mtu makini na mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya Uwekezaji. Hii ndiyo sababu kubwa ya Serikali kuamua kumpeleka Mkoani Mtwara kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuwaandaa Wananchi kwa fursa zinazokuja. Nina hakika kuwa, baada ya mapatano hayo, Mkoa utarejea katika hali yake ya kawaida na kufanya kazi kwa karibu na Uongozi wa Mkoa kwa maendeleo yao.

  SUALA LA MPASUKO WA VIONGOZI WA MKOA WA MTWARA

Mheshimkiwa Spika,
Nimesikitika kusikia kuwa katika Mkoa wa Mtwara, Viongozi wake wa Kisiasa wana mpasuko ambao kwa maoni ya Wananchi, umesababisha kurudisha nyuma maendeleo ya Mtwara. Ninachoweza kusema kwa sasa ni kuwasihi Viongozi wenzangu wa Bunge na wale wa Chama kukaa chini na kuondoa tofauti zao kwa lengo la kuusaidia Mkoa wa Mtwara. Tofauti hizi ndizo zilizosababisha hata madhara na hasara kwa baadhi ya Viongozi kama tulivyoshuhudia. Hali hii ni ya hatari na isiyopendeza kwa Jamii. Chuki na tofauti kati yetu hazina budi kukomesha, kwani lengo letu siku zote kama Viongozi ni kuwahudumia na kuwasikiliza Wananchi. Hali iliyopo Mkoani Mtwara baina ya Wananchi na Viongozi wao si ya kuridhisha, na hivyo ni wajibu wa Viongozi na wana Mtwara wenyewe kurekebisha hali hii na kusonga mbele.

3.0 MAPENDEKEZO YA SERIKALI

Mheshimiwa Spika,
  Ili kuhakikisha kuwa Wananchi wanakuwa na uelewa sahihi wa Mradi huu na Miradi mingine iliyopo na itakayokuwapo Mkoani Mtwara, nimeushauri Uongozi wa Mkoa uunde Kamati Maalum ya Kusimamia na Kusukuma Maendeleo ya Mkoa wa Mtwara. Kamati hii itakuwa na jukumu la kufuatilia maendeleo ya Miradi mbalimbali Mkoani na kutoa elimu kwa Miradi inayohusu Wananchi kwa kushirikiana na Wataalam. Lengo likiwa kuwafikishia Wananchi taarifa sahihi za Miradi inayowahusu.


Kamati hiyo itakayokuwa nje ya Mfumo wa Serikali, itajumuisha Wajumbe kutoka Sekta Binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Madhehebu ya Dini, n.k. ambapo Serikali itakuwa ikisaidia na kutoa msukumo pale itakapohitajika.

  Kutokana na maendeleo ya Gesi Mkoani Mtwara, Serikali inawashauri Wana-Mtwara kutambua fursa walizonazo na kujipanga katika masuala yafuatayo:


  Kutokana na vurugu zilizotokea Mkoani Mtwara, ninatoa wito kwa Wananchi wa Mtwara kuwa, maadam sasa Viongozi wa Mkoa huo kwa kupitia makundi mbalimbali niliyokutana nayo wameshaeleweshwa suala hili la Mradi wa Gesi vizuri, sasa ni wajibu wao kuwaelewesha Wananchi wao kuhusu suala hili! Lengo likiwa ni kuwaelimisha ili vurugu zilizotokea na kuleta madhara makubwa zisitokee tena. Ninapenda kuwashauri kuwa, endapo kuna tatizio limetokea, basi ni vizuri kukaa na Viongozi wao na kuliwasilisha ili lipatiwe ufumbuzi. Wanapoharibu miundombinu ya Umma ambayo imejengwa kwa fedha zao wenyewe kama walipa kodi ni kujikomoa wenyewe kwani nao watakosa huduma muhimu watakazohitaji. Katika matukio haya ni kama vile kukosa huduma za magari ya wagonjwa, huduma za Mahakama, n.k.

Vilevile, tabia ya Kikundi cha Wananchi kujichukulia hatua mkononi na kuharibu mali za Umma na za Watu binafsi haitavumiliwa. Wale wote wenye kufanya vitendo kama hivyo, watachukuliwa hatua stahiki.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,
Faida za gesi iliyopatikana Nchini mwetuna ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ni nyingi, kwa uchache naomba kuzitaja kama ifuatavyo:

  Kuwepo kwa miundombinu madhubuti ya usafirishaji wa gesi kutoka ilikogundilika kwenda kwenye maeneo mengine ya Nchi kwa matumizi ya kiuchumi na kufanya Nchi yetu kuwa ya uchumi wa gesi ;


  Kuwezesha uzalishaji wa haraka wa umeme nchini ambao ni zaidi ya MW 2500 kabla ya mwaka 2015 na hivyo kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi ;


  Kuimarika kwa Sekta ya Viwanda kutakako sababishwa na uwepo wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu. Kwa sasa bei ya umeme ni Dola za Marekani senti 35 - 45 kwa uniti, wakati umeme utakaozalishwa na gesi utauzwa kwa kati ya Dola za Kimarekani senti 6 - 8 kwa uniti.
  Kuokoa zaidi ya kiasi cha shilingi Trilioni 1.6 kwa mwaka zinazotumika kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalishia umeme.


  Kutokana na matumizi ya gesi asilia kwenye magari, mahotelini, na majumbani kwa Dar es Salaam peke yake zitaokolewa zaidi ya shilingi Bilioni 320 kwa mwaka, na kiwango hicho kitaongezeka kulingana na kuongezeka kwa matumizi ya gesi badala ya mafuta kwa eneo kubwa zaidi la Nchi.


  Kuongezeka kwa ajira katika sekta mbalimbali, maana usalama wa ajira kwa miaka ya karibuni uliathiriwa zaidi na kutokuwepo kwa umeme wa uhakika ;


  Kuimarika kwa Sekta ya Kilimo kutokana na kuwepo kwa mbolea yenye bei nafuu itakayozalishwa Nchini ; na


  Kuwa na usalama wa mazingira yetu kutokana na matumizi ya gesi asilia kupikia badala ya kutumia mkaa na kuni, n.k.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote wa Tanzania kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za dhati za matumizi ya gesi kutoka Mtwara kwa manufaa mbalimbali ikiwemo kutatua tatizo kubwa la nishati ya umeme Nchini ili tuweze kujenga Nchi yenye uchumi wa Viwanda kwa ustawi wa Wananchi wote wa Tanzania.

Ninawasihi WanaMtwara wawe na umoja na subira katika suala hili la Gesi wakati Serikali ikikamilisha taratibu zitakazowezesha Wananchi kuona matunda ya rasilimali hii ya Gesi.


Watanzania hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya rasilimali ya Gesi aliyotupatia. Ni vyema tukahakikisha kwamba, baraka hii haigeuki kuwa laana kwetu na kwa vizazi vijavyo, bali iwe ni mwanzo wa neema kwetu, na kwa vizazi vyetu. Umoja wetu kwa wakati huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mwisho, napenda kuchukua kuchukua fursa hii kuwashukuru Mawaziri Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi (Mb.), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb.), Waziri wa Uchukuzi; Mheshimiwa Prof. Anna Tibaijuka (Mb.), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; na Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa (Mb.), Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kuambatana nami Mkoani Mtwara na kutoa maelezo na ufafanuzi katika maeneo ya Sekta zao. Maelezo hayo yamekuwa ya msaada mkubwa, kwani naamini yamesaidia kutoa uelewa kwa Wananchi wa Mkoa wa Mtwara kupitia Viongozi wao.

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
All the contents on this site are copyrighted ©.