2013-01-31 08:58:21

Majadiliano, ukweli, uwazi na demokrasia ni mambo msingi katika kudumisha haki, amani na utulivu


Maaskofu Katoliki wa Croatia, waliokuwa wamekutanika mjini Zagbreb hivi karibuni, wamehitimisha Maadhimisho ya Siku ya 53 ya Taalimungu ya shughuli za kichungaji, kwa kutoa tamko linalokazia umuhimu wa majadiliano kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wananchi wa Croatia, hususan katika masuala yanayohusu: elimu ya afya; amani na utulivu pasi na vitisho dhidi ya Kanisa na kwamba, Serikali inapaswa kumheshimu mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kutambua na kuheshimu maisha ya ndoa na familia.
Washiriki wa maadhimisho haya wanaiomba Serikali ya Croatia kuonesha utayari wa kufanya majadiliano ya kina kuhusu mpango mkakati wa kutaka kuanzisha elimu ya afya ya uzazi; kwa kufanya mabadiliko katika maamuzi yaliyotangulia, ili kudumisha haki msingi za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria, bila kusahau dhamana na wajibu wa wazazi katika kuwalea watoto wao katika imani, maadili na utu wema; haki na wajibu ambao wamepewa Kikatiba.
Elimu ya uzazi salama haiwezi kufundishwa shuleni pasi na kupata ridhaa ya wazazi wanaopaswa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata elimu na makuzi sahihi yatakayowawezesha kufikia ukomavu katika maisha na utu wao! Ili kupata mafao ya wengi na kufikia malengo haya, kuna haja ya wadau wa sekta ya elimu kushirikiana kwa karibu zaidi na wazazi pamoja na walezi.
Wajumbe hao wanabainisha kwamba, uamuzi wa Serikali kuanzisha utoaji wa elimu ya afya uzazi bila ya kuwashirikisha ni kwenda kinyume cha Katiba ya nchi inayotoa haki na uhuru kwa wazazi pamoja na watoto wao. Kwa bahati mbaya, mwelekeo huu umesababisha kinzani na mgawanyiko nchini Croatia, jambo ambalo lina madhara makubwa katika elimu.
Ni matumaini ya wajumbe hao kwamba, mantiki itaweza kutawala badala ya kutumia mabavu ili kulazimisha ajenda tata zinazotaka kukumbatia utamaduni wa kifo. Majadiliano, ukweli, uwazi na demokrasia ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu kwa kuheshimu pia Katiba ambayo kimsingi ni Sheria Mama.







All the contents on this site are copyrighted ©.