2013-01-31 09:16:52

Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani ni kielelezo cha mshikamano na wanaoteseka na magonjwa!


Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, kunako tarehe 13 Mei 1992 alianzisha Siku ya Wagonjwa Duniani, kwa lengo la kutaka kuwahamasisha Watu wa Mungu, Taasisi za huduma ya afya, Jamii na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, inatoa huduma bora na makini kwa wagonjwa. Kwa mara ya kwanza, Siku hii ikaadhimishwa kunako tarehe 11 Februari 1993 kwenye Madhabau ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa.

Na tangu wakati huo maadhimisho haya yamekuwa daima yakichukua sura ya kimataifa kwa kuadhimishwa huko Lourdes, Vatican, Asia, Oceania, Ulaya na Afrika. Ni maadhimisho ambayo yanaandaliwa kati ya Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa Sekta ya afya. Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Monsinyo Jean Marie Mupendawatu, Katibu mkuu Baraza la Kipapa la huduma ya kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, walipokuwa wanazungumza na waandishi wa habari, hivi karibuni.

Anasema, Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani ni muda wa: sala, tafakari ya kina, pamoja na kushirikishana uzoefu, ujuzi na mang’amuzi kuhusu mateso na mahangaiko ya wagonjwa wanaoonesha ile sura ya Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Maadhimisho haya yanafanyika katika maeneo makuu matatu: kwanza kabisa ni muda wa Liturujia ya Kanisa: hapa waamini wanapata nafasi yak usali, kutafakari Neno la Mungu pamoja na kuadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Mpako wa Wagonjwa.

Pili ni kipindi cha kuangalia changamoto za kichungaji na matendo ya huruma: Hapa waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, Siku ya Wagonjwa Duniani wanaitumia kwa ajili ya kuwatembelea na kuwahudumia wagonjwa walioko kwenye familia, waliolazwa hospitalini au wanaotunzwa kwenye nyumba za wazee na vituo maalum. Ni vyema ikiwa kama wahudumu wa wagonjwa wataweza pia kupata fursa ya kuzungumza na wahudumu na viongozi katika sekta ya afya kwenye eneo husika.

Ni muda pia wa kuweza kukutana na vyama na watu wanaotoa huduma ya kujitolea kwa wagonjwa, ili kwa pamoja kuweza kumshukuru Mungu kwa Siku hii maalum. Pale inapowezekana, viongozi wa Serikali na wanasiasa washirikishwe ili waweze kutoa mchango wao chanya katika huduma kwa wagonjwa.

Tatu ni kipindi cha tafakari ya kina kwa kuangalia mikakati ya shughuli za kichungaji katika sekta ya afya kama zinavyobainishwa na Kanisa mahalia, daima mgonjwa akipewa kipaumbele cha kwanza kama alivyobainisha Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, tangu siku ile ya kwanza ya Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani. Maandalizi haya kwanza kabisa yanapaswa kugusa dhamiri za watu, ili hatimaye, waweze kuchangia katika ujenzi wa haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati na wagonjwa. Hata katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu, bado kuna kinzani na ukakasi unaojionesha katika kuwahudumia wagonjwa.

Monsinyo Jean Marie Mupendawatu, anasema, inasikitisha kuona kwamba, bado kuna idadi kubwa ya watu wanaopoteza maisha yao Barani Afrika, Asia na katika baadhi ya nchi za Ulaya kutokana na ukosefu wa miundo na huduma bora za afya. Lakini, maendeleo haya huko Marekani na Barani Ulaya yanaanza kuwa nitishio la zawadi ya maisha, kwa watu kutaka kukumbatia mno utamaduni wa kifo.

Hospitali na vituo vya afya anasema Baba Mtakatifu ni Majukwa makini ya Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hii ni changamoto kwa waamini kujitoa kimasomaso katika mchakato wa Uinjilishaji, hata katika nyakati hizi ambamo makucha ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa yanaendelea kusikika kila pembe ya dunia, Rasilimali iliyopo itumike barabara kwa ajili ya mafao ya wengi na hasa zaidi kwa kuwahudumia wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Ikumbukwe kwamba, afya ni haki msingi ya binadamu na kamwe haiwezi kugeuzwa kuwa ni bidhaa. Utu na heshima ya mgonjwa vinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote! Waamini na watu wenye mapenzi mema, wasimame kidete dhidi ya utamaduni wa kifo unaotishia zawadi ya uhai. Monsinyo Jean Marie Mupendawatu anahitimisha mchango wake kwa kusema kwamba, kuna haja kwa wadau mbali mbali katika sekta ya afya kushirikiana kwa dhati wakiongozwa na kanuni auni; utu na heshima ya mwanadamu vipewe kipaumbele cha kwanza.
All the contents on this site are copyrighted ©.