Haki na amani ni mambo yanayoendelea kutikisa maisha ya watu sehemu mbali mbali za
dunia!
Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, kusherehekea matunda ya miaka
hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
juu ya Uinjilishaji Mpya iliyofanyika mjini Vatican, Oktoba 2012 ni wakati muafaka
kwa Mama Kanisa kuendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu misingi ya haki na amani;
mambo yanayoendelea kugusa maisha ya watu wengi duniani. Haki na Amani
ni chanda na pete na mwaliko wa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, kuonja upendo na ukarimu huu unaopata chimbuko lake katika kweli
za Kiinjili, kama zilivyotangazwa na Yesu Kristo mwenyewe. Ni mambo msingi yanayopaswa
kufanyiwa kazi katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kujikita katika toba na wongofu
wa ndani. Pengine umefika wakati wa kumwilisha kwa kasi zaidi uelewa wa haki jamii,
kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa katika utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji
Mpya, inayovaliwa njuga wakati huu wa Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni
mchango wa Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani wakati
wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya. Anasema kwamba, Uinjilishaji
Mpya ni nyenzo ya Uinjilishaji inayopania kuwaonjesha watu ile furaha ya imani na
upendo; mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza kama mdau na mlengwa wa maendeleo
ya mwanadamu. Uinjilishaji Mpya unapaswa kuwa ni dhamana endelevu, ili kuweza
kuleta mabadiliko yanayokusudiwa na Mama Kanisa katika Jamii, hasa katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwani kuna kinzani nyingi kuhusu
mwono na uelewa wa mwanadamu. Hali hii inaonesha haja ya kuanza kwa bidii mchakato
wa Uinjilishaji Jamii kama mwendelezo makini wa Uinjilishaji; jambo ambalo ni changamoto
endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Peter Turkson anasema, leo
hii kuna watu wanauelewa mpana na wanaguswa kwa karibu sana na tema kama vile: haki
msingi za binadamu; mafao ya wengi, ekolojia na mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi
na ubadhirifu wa mali ya umma kama kikwazo kikubwa cha maendeleo endelevu ya binadamu.
Ni mambo tete yanayogusa maisha ya mtu binafsi na maisha ya Jumuiya ya Kimataifa;
changamoto kwa Kanisa kujikita katika Uinjilishaji Jamii. Ili kuweza kufikia malengo
haya anasema Kardinali Peter Turkson, kuna haja ya kujikita katika majiundo ya awali
na endelevu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ili waweze kufahamu kwa kina
mapana Mafundisho Jamii ya Kanisa; muhtasari wa vitendea kazi kwa waamini walei katika
dhamana ya kuyatakatifuza malimwengu. Kardinali Turkson anasema kwamba, kati ya
Nyaraka ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi kwa sasa ni Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki,
Nyaraka za Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Mafundisho Jamii ya
Kanisa. Kwa mantiki hii, Kardinali Turkson analihamasisha Kanisa Katoliki kuangalia
uwezekano wa kuadhimisha Sinodi juu ya Uinjilishaji Jamii kwa siku zijazo.