2013-01-31 07:51:11

Dr. Asha Rose Migiro ateuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania


Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Dk. Asha Rose Migiro kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Taarifa iliyotolewa Dare Es Salaam na kutiwa saini, Jumatano, Januari 30, 2013 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza Januari 17, 2013.

Mheshimiwa Asha Rose Migiro ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Katibu wa NEC wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Aidha, Dkt. Migiro amepata kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania.

Wakati huo huo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Pius Makuru Nyambacha kuwa Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania. Taarifa iliyotolewa mjini Dar Es Salaam na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, Januari 30, 2013 inasema kuwa uteuzi wa Bwana Nyambacha ulianza Jumanne ya Januari 22, mwaka huu, 2013. Aidha, taarifa hiyo inasema kuwa kabla ya uteuzi wake, Bwana Nyambacha alikuwa Kaimu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
All the contents on this site are copyrighted ©.