2013-01-31 08:25:49

Baba wa Taifa alithamini na kuheshimu uhuru wa kidini, akakazia umoja na mshikamano wa kitaifa!


Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa ni Mchamungu na alipenda kusali na kuwaona watanzania wenzake wakiabudu na kukiri imani kadiri ya dini na madhehebu yao, kama njia ya kukuza na kudumisha uhuru wa kidini, ambayo ni haki msingi ya kila mwanadamu. RealAudioMP3
Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania anasema kwamba, Mwalimu Nyerere baada ya kung’atuka kutoka madarakani, alitamani kujenga Kanisa ili aweze kupata mahali pa kusali, karibu na nyumbani kwake Kijijini Butiama. Alifanikiwa kupata msaada wa fedha, akajenga Kanisa la Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Yesu, ambalo kwa sasa ni Kanisa la Parokia ya Butiama, Jimbo Katoliki Musoma.
Baba wa Taifa aliguswa mno na mahitaji ya Waamini wa dini ya Kiislam, Kijijini Butiama, akatafuta msaada wa fedha ili kuwajengea Msikiti mkubwa na mzuri, ambao hadi leo hii umebaki kumbu kumbu tosha kabisa kwamba, kwa hakika Mwalimu Nyerere alikuwa ni mtu aliyejikita katika majadiliano ya kidini, akaheshimu uhuru wa kidini. Askofu Msonganzila anasema, msaada wa ujenzi wa Msikiti wa Butiama kwa Baba wa Taifa ni mchango kutoka kwa Hayati Mohamed Ghaddafi wa Libya.
Kumbe, uvumi kwamba, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwanyanyasa na kuwabeza waamini wa dini ya Kiislam nchini Tanzania hauna msingi wowote ni njama za kutaka kuvuruga amani, utulivu na mshikamano wa watanzania. Mwalimu Nyerere alikazia zaidi na zaidi umoja na mshikamano wa kitaifa, akapinga kwa nguvu zote ukabila, udini na ubaguzi.
Miaka michache tu baada ya kifo chake, watanzania wameanza kubaguana kwa misingi ya: itikadi na vyama vya kisiasa, wakanuniana! Wameingia katika misimamo mikali ya kidini: wakaanza kuchomeana Makanisa. Wameanza pia kubaguana kwa “Mabucha ya nyama”, jambo ambalo halikuwa na uzito wa pekee miaka kadhaa iliyopita, watanzania waliheshimiana na kuthaminiana kwa tofauti zao za Kiimani, wakatambuana kuwa wao jambo la msingi ni Utanzania unaowaunganisha na wale si kabila wala dini ya mtu!
Mtwara kunafuka moto! Rasilimali na utajiri wa nchi ambao unapaswa kuwa ni mali ya watanzania wote unawagawa watanzania! Watanzania wanakoelekea si pazuri!
Akiwa mjini Addis Ababa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amesikika akisema “Nakaribisha kwa mikono miwili pendekezo la APRM kuwa serikali isimamie kwa uangalifu tofauti za kidini nchini. Kama mnavyojua, Tanzania imekuwa na amani na utulivu kwa sababu tumekuwa na bahati kutokuwa na ugomvi wa kikabila, kidini ama yale ya kutokana na rangi za watu. Hali hii inatokana na ukweli kuwa tumetunga na kuwa na sera zisizokuwa za kibaguzi kwa wananchi wetu kwa misingi ya kabila, dini, rangi ama sehemu anakotoka Mtanzania. Ni sera nzuri na tutazidumisha.”
Aliongeza: “Uzuri kuhusu dini katika Tanzania ni kwamba tunaamini na kudumisha uhuru wa kuabudu kwa kila mtu. Serikali haina dini. Lakini tunajua fika kuhusu hatari zinazoweza kusababishwa na wanasiasa na viongozi wa dini wenye malengo ya kuchochea fujo za kidini. Hatutayumba wala kusita kupambana ipasavyo na watu wa namna hiyo. Pale ambako uchochezi wa kidini unafikia kiwango cha kuhatarisha amani ya nchi ama uvunjifu wa amani na sheria, dola ina haki ya kuingilia kati.”








All the contents on this site are copyrighted ©.