2013-01-30 10:56:14

Waamini waone, waguswe na kutenda kama Msamaria mwema kwa kuwahudumia wagonjwa!


Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013 yanayoongozwa na kauli mbiu "Nenda nawe ukatende vivyo hivyo" yaanza rasmi hapo tarehe 7 hadi tarehe 11 Februari 2013 kwenye Madhabau ya Bikira Maria Altotting, Ujerumani. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho haya anawakilishwa na Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la Wahudumu wa Sekta ya Afya.

Akizungumza na waandishi wa Habari, hapo tarehe 29 Januari 2013, Askofu mkuu Zimowski anasema, maadhimisho haya ni kipindi maalum kwa ajili ya kutafakari na kurudia tena majitoleo ya Mama Kanisa kwa ajili ya wagonjwa, wahudumu na wote wanaoteseka kiroho na kimwili; ili kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Kristo kwa njia ya Sala, Tafakari ya kina pamoja na kutolea mateso yao kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa Siku ya 21 ya Kuombea Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013.

Ni mwaliko wa kuitazama ile sura ya Kristo: aliyeteseka, akafa na kufufuka kutoka katika wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Injili ya Msamaria mwema iwe ni kielelezo na changamoto makini kwa waamini kutekeleza haya kwa wagonjwa na wote wanaoteseka, ili waweze kweli kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kwa maneno mengine ni changamoto ya kila mwamini kuwa ni Msamaria mwema kwa jirani na katika mazingira yake.

Uwezo na nguvu hii inapaswa kwanza kabisa kuwa ni kielelezo cha imani thabiti inayopata chimbuko lake katika maisha ya mwamini mara baada ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yake ya kila siku. Msamaria mwema ni chachu ya upendo ndani ya Jamii, mwaliko na changamoto ya pekee kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani.

Watu waone, waguswe na kutenda kama alivyofanya yule Msamaria mwema, wakijitahidi pia kuiga mifano ya watakatifu mbali mbali waliyoyamimina maisha yao kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia.All the contents on this site are copyrighted ©.