Utu na heshima ya mwanadamu vipewe kipaumbele cha pekee katika sera za wahamiaji na
watu wasiokuwa na makazi
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao makuu yake hapa mjini Roma, tarehe 29 Januari
2013 imefanya Kongamano lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu "wahamiaji na mshikamano
wa kiimani". Kongamano ambalo limehudhuriwa pia na na Kardinali Antonio Maria Veglio',
Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa
na makazi maalum.
Katika kongamano hili, Serikali ya Romania ilimpatia Kardinali
Veglio' nishani, kwa kutambua mchango wake katika kulinda na kutetea haki msingi za
wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum sehemu mbali mbali duniani. Anasema,
ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unaonesha utajiri na
tofauti kubwa zinazojionesha miongoni mwa watu: kitamaduni, kijamii, kiuchumi, kisiasa
na hata kidini, kiasi kwamba, hata hali ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum
wanakuwa mashakani.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anaonesha imani
na matumaini ya pekee kwa wahamiaji kama mahujaji wa imani na matumaini, licha ya
Njia ya Msalaba wanayokabiliana nayo katika hija ya maisha yao. Wananchi wa Romania
wanakabiliwa pia na tatizo la wananchi wanaolazimika kuyahama makazi yao ili kutafuta
hali bora zaidi ya maisha katika nchi nyingine; huko wanakumbana na hali ngumu kutokana
na hofu za vitendo vya kigaidi, biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya; ukahaba
pamoja na vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu.
Katika hali
zote hizi, utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza anasema
Kardinali Veglio'. Wahamiaji ni rasilimali ambayo ikitumiwa vyema inaweza kuwa ni
msaada mkubwa katika maendeleo kwenye medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.