Mheshimiwa Padre Marco Tasca achaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wafranciskani
Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisco, katika maadhimisho ya Mkutano mkuu
wa mia mbili, wamemchagua Mheshimiwa Padre Marco Tasca kuwa Mkuu wa Shirika kwa kipindi
cha miaka sita, baada ya kupewa siku kumi za kusali, kutafakari na kupembua maisha
yake na sasa anajikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwaongoza ndugu
zake katika maisha na utume wa Shirika.
Ni mwaliko na changamoto ya pekee kwanza
kabisa: kulifahamu, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu kama kielelezo cha
Imani tendaji kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Mheshimiwa Padre
Tasca anamwomba Mtakatifu Francisco wa Assis awaombee neema na baraka za kuweza kuwa
kweli ni mashahidi wa imani na matumaini, wakijitahidi kuiga mfano na maisha ya Mtakatifu
Francisco wa Assis.
Ni mwaliko kwa Wafranciscan kuendelea kuwa ni wajumbe wa
amani na upatanisho, changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi kutokana na vita,
kinzani na migogoro inayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Ni ushuhuda
unaopaswa kujikita katika uhalisia wa maisha ya Wanashirika hawa.
Ni muhimu
pia kuendeleza mchakato wa utamadunisho, kwani Shirika lina watu kutoka sehemu mbali
mbali wanaotekeleza utume wao pia sehemu mbali mbali za dunia, bila kusahau majadiliano
ya Kiekuemene na Kidini na Waamini wa dini ya Kiislam. Ushuhuda wa kwanza kadiri ya
Sheria za Wafranciskani unajikita katika mahusiano mema!