2013-01-30 07:35:10

Majadiliano ya kidini na kiekumene ni njia muafaka katika utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji Mpya!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, hivi karibuni, limehitimisha mkutano wake wa mwaka, uliofanyika kwa mara ya kwanza katika historia yake nchini Vietnam. RealAudioMP3

Tukio hili ni baraka kwa Bara la Asia na Kanisa katika ujumla wake, kwani Shirikisho hili linaadhimisha miaka arobaini tangu lilipoanzishwa ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa Barani Asia.

Wajumbe walipata fursa ya kuangalia na kupembua maisha na utume wa Kanisa katika nyanja mbali mbali za maisha, lakini zaidi wamejikita katika majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali Barani Asia; uhuru wa kidini ambao umekuwa na utata katika nchi nyingi Barani Asia kutokana na baadhi ya waamini kuwa na misimamo mikali ya kiimani inayotishia amani na usalama wa raia na mali zao. Maaskofu wamepembua kwa kina na mapana dhana ya umaskini na mapambano yake, ili kuboresha idadi kubwa ya watu wanaoendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato.

Maaskofu wameona pia kwamba, kuna changamoto kubwa mbele yao ya kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda na kuwatetea wazawa; wameangalia hali ya wahamiaji na wakimbizi wanaoyakimbia makazi yao kutokana na sababu mbali mbali na jinsi ya kuwahudumia. Hadi hapa Maaskofu walikuwa wanajadili kuhusu hali ya maisha ya kijamii na kisiasa Barani Asia.

Maaskofu wamezama kwa undani zaidi kwa kuangalia dhamana na nafasi ya waamini walei katika ushuhuda wa maisha na changamoto wanazokabiliana nazo katika kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; pamoja na kushiriki kikamilifu katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kurithisha imani kwa njia ya ushuhuda wa furaha ile inayobubujika kutoka katika undani wa waamini wanaokutana na Yesu katika hija ya maisha yao: kwa njia ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti bila kusahau matendo ya huruma ambayo kimsingi ni Imani katika matendo.

Wajumbe kutoka Mabaraza mbali mbali ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, walipata fursa ya kuelezea hali ya maisha, utume, changamoto na matatizo wanayokabiliana nayo katika kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili. Changamoto kubwa ambayo imeguswa na wengi ni umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali Barani Asia kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kama walivyokazia Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya, iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican.

Baadhi ya wajumbe wamekiri pia umuhimu wa majadiliano ya kiekumene na waamini wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo ambayo yanaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa, kwa kujikita katika kuwapatia watu majibu ya mkato kutokana na shida na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo! Jambo la msingi wanasema wajumbe, ni kujenga mazingira ya kuaminiana, kuheshimiana na kuthaminiana, wote kwa pamoja wakipania kutafuta mafao ya wengi, kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Kumekuwepo na dalili nzuri za majadiliano kati ya Kanisa na Serikali ya Vietnam na kwamba, kuna dalili za maboresho ya uhusiano kati ya Kanisa na Serikali ya China, ingawa bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kutekeleza.

Wakristo Barani Asia wanahitaji kwa namna ya pekee kuchangamka ili kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, katika utamaduni na mazingira ambayo yanaonesha kuwa na changamoto hasi. Wazawa wanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa pamoja na kuwezeshwa katika sekta mbali mbali za maisha, ili waweze kutekeleza vyema nyajibu zao katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii inayowazunguka.

Kuna hatari kwamba, mbegu ya utamaduni wa kifo inaendelea kupandikizwa kwa kasi ya ajabu Barani Asia, kwa hofu kwamba, kuna idadi kubwa ya watu wanaongezeka siku hadi siku, hapa waamini wanapaswa kukumbatia na kuenzi Injili ya Uhai. Kuna madhara makubwa ambayo yametokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo imepelekea watu wengi hasa kutoka Bangaladesh kuishi katika mazingira magumu ya kiuchumi na kijamii; wengi wanaendelea kutumbukia katika lindi la umaskini wa hali na kipato.

Katika mazingira kama haya, utume wa Kanisa unajikita zaidi na zaidi katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili; kwa kuenzi utu na heshima ya kila mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; kusimama kidete kupinga rushwa, ubadhilifu wa mali ya umma na ufisadi, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaonesha ubinafsi wa baadhi ya watu ndani ya Jamii; hali inayoweza pia kuchangia kuporomoka kwa misingi ya haki, amani na utulivu.

Kanisa Katoliki Barani Asia linapenda kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, likitambua dhamana na sauti yake ya kinabii; dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini au Eutanasia kama kinavyojulikana na wengi.

Mwishoni, wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Asia wamekazia umuhimu wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikrsto kama shule ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma yanayojenga na kuimarisha Injili ya Upendo na Mshikamano; kielelezo makini cha ushuhuda wa Imani katika matendo.
All the contents on this site are copyrighted ©.