2013-01-30 13:53:43

Katekesi ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI: Kanuni ya Imani: Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi!


Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi ndiyo sehemu ya Katekesi ambayo imefafanuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 30 Januari, kwenye Ukumbi wa Papa Paulo wa VI mjini Vatican.

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu ameanza katekesi makini kuhusu Kanuni ya Imani inayomwonesha Mungu kuwa ni Baba na Mwenyezi, licha ya kinzani zinazojitokeza katika Jamii ya leo hii kuhusu Ubaba, lakini bado Maandiko Matakatifu yanafafanua maana halisi ya kumwita Mwenyezi Mungu kuwa "Baba".

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa ukarimu, mwaminifu na mwenye kusamahe na kuupenda ulimwengu, kiasi hata cha kumtoa Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo kuja ulimwenguni kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yesu Kristo ni sura ya Mungu asiyeonekana ambaye amewafunulia watu kuwa ni Mungu Baba mwenye huruma ambaye kamwe hawachi watoto wake, anawapenda kiasi hata cha kukumbatia Fumbo la Msalaba.

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo amewafanya watu wote kuwa ni watoto wake na kwamba, Msalaba unaonesha ukuu wa Mungu unaovuka ufahamu na uelewa wa binadamu. Ukuu wake unafumbata kwa namna ya pekee, upendo unaovumilia unaojionesha kwa wema kushinda uovu; uhuru wa kweli dhidi ya utumwa wa dhambi. Waamini wanapolitafakari Fumbo la Msalaba wa Kristo, wanahamasishwa kumgeukia Mwenyezi Mungu na kuomba neema, imani, matumaini, upendo na nguvu yake inayookoa.

Mwaka wa Imani iwe ni fursa kwa waamini kutambua kwamba, kweli Mwenyezi Mungu ni Baba, ukweli ambao unawachangamotisha waamini kuwa ni mashahidi wenye furaha kwa Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; wakati wa raha na uchungu, kwani Mwenyezi Mungu yuko daima pamoja na watu wake, anawaongoza na kuwatakia mema.

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa Maaskofu Marafiki wa Chama cha Wafokolari kutoka sehemu mbali mbali za dunia walioanza mkutano wao hapo tarehe 29 Januari na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 31 Januari 2013. Maaskofu hawa pamoja na mambo mengine, wanatafakari kuhusu: uinjilishaji, tasaufi ya umoja na mshikamano, changamoto za kipindi cha mpito Barani Ulaya, Wafokolari na Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ni fursa ya kutolea ushuhuda katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu akitambua kwamba, wakati huu kuna Vyama mbali mbali vya kitume vinavyoendelea kukutana, amewatakia wote keri na baraka tele katika maisha na utume wao, daima wajitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano. Anawataka viongozi wa Kanisa kuimarisha Katekesi kwa vijana wa kizazi kipya wanaojiandaa kupokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa, ili waamini waweze kukua na kuimarika katika imani.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 31 Januari, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco, Padre na Mlezi wa Vijana. Awe ni mfano wa kuigwa katika maisha ya vijana; wagonjwa wachote uzoefu na mang'amuzi yake ya maisha ya kiroho katika hija ya maisha yao, kwa kujiaminisha kwa Kristo. Wanandoa wapya wakimbilie katika maombezi yake ili kuishi kikamilifu ile karama ya pendo na utume wa wanandoa.All the contents on this site are copyrighted ©.