2013-01-29 07:29:35

Tafakari kwa Mababa wa Sinodi ya Kanisa la Caldea ya Babiloni


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, amewahakikishia Mababa wa Sinodi ya Kanisa la Caldea ya Babiloni, wanaoendelea na maadhimisho ya Sinodi yao, uwepo wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa njia ya sala, wakati huu wanapojipanga kwa ajili ya kumchagua Patriaki mpya, atakayechukua nafasi ya Patriaki Emmanuel Delly wa tatu, aliyeliongoza Kanisa kwa busara na moyo mkuu katika kipindi kigumu ndani na nje ya nchi yake.

Mababa wa Sinodi hii wanashiriki kikanmilifu maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu licha ya kuwa na: Sheria, Liturujia na Mapokeo ya Makanisa ya Mashariki, lakini wote wanatekeleza dhamana yao kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uchaguzi wa kiongozi mkuu wa waamini wa Caldea ya Babiloni ni muhimu sana kwa Kanisa lenyewe, Mapokeo, Urithi na Utajiri pamoja na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi.

Kiongozi atakachaguliwa anapaswa kuwa ni mhimili mkuu wa maisha ya kiroho, kisakramenti na kichungaji, daima akijikita kutafuta umoja wa Kanisa. Uchaguzi huu unafanyika wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Mwaka wa Imani, mwaliko wa kutambua kwamba, kwa hakika imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; inapaswa kufahamika, kuendelezwa na kutolewa ushuhuda makini.

Ni uchaguzi unaofanyika kwa uhuru kamili, wakitambua kwamba, wanatekeleza dhamana hii mbele ya Mungu na kwamba, kura zinapaswa kumwendea kiongozi anayeweza kubeba dhamana hii kwa ajili ya utukufu wa Mungu na mafao ya Kanisa.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Enrico Dal Covolo, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, akitoa tafakari yake kwa Mababa wa Sinodi hii, amewataka kufuata mfano wa Kanisa la Mwanzo lililokuwa limekutanika mjini Yerusalem, kama kielelezo cha umoja unaopaswa kujionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya kiroho na kimwili, kwani waamini wa Kanisa la Mwanzo walikuwa na mwili mmoja na roho moja.

Ujumbe ambao anaendelea pia kuukazia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Kanisa Mashariki ya Kati. Ni mwaliko wa kujikita katika kufundisha, kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini katika kuumega Mkate na Maisha ya Sala. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kukua na kuendelea kuongezeka siku hadi siku.
All the contents on this site are copyrighted ©.