Patriaki Bechara Boutros Rai kutoa tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya
Colosseo, Ijumaa kuu, 2013
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, akiwa bado na kumbu kumbu hai ya hija yake
ya kichungaji nchini Lebanon ili kuzindua matunda ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Mashariki
ya Kati, ameamua kumkabidhi tafakari ya Njia ya Msalaba wakati wa Ijumaa kuu usiku,
kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Patriaki Bechara Boutros Rai.
Hii
itakuwa ni fursa nyingine kwa Mama Kanisa kufanya Njia ya Msalaba na Waamini wanaoishi
Mashariki ya Kati, ili kuonja matumaini, mateso na mahangaiko yao ya kila siku. Taarifa
ya uteuzi huu inafafanua kwamba, tafakari hii, itaandaliwa na vijana wawili kutoka
Lebanon ina watafuata Vituo vya Njia ya Msalaba kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, yaani
Vituo 14.
Itakumbukwa kwamba, kwa mwaka huu, 2013, Ijumaa kuu, Siku kuu ya
Mateso na Kifo cha Kristo Msalabani, itaadhimishwa hapo tarehe 29 Machi 2013.