2013-01-29 08:04:13

Mpasuko wa kidini unaweza kuitumbukiza Tanzania katika janga la kitaifa!


Amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa ambao watanzania wamejivunia kwa takribani miaka 50 unaanza kuingiwa na dosari kubwa kutokana na kushamiri kwa vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani unaokumbatiwa na udini pamoja na misimamo mikali ya kiimani.

Kuna mikakati ya makusudi kabisa inayofanywa ili kuweza kuitumbukiza Tanzania katika machafuko ya kidini kwa kutumia mgongo wa kidini. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania wakati akijibu hoja zilizoibuliwa katika taarifa ya tathmini ya Mpango wa Afrika Kujitathmini kiutawala Bora, iliyowasilishwa mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Kuna changamoto kubwa kwamba, nchini Tanzania kumeaanza kuonekana mpasuko mkubwa wa kidini hali inayotishia: utulivu, amani, mshikamano na maendeleo endelevu. Rais Kikwete ameonya kwamba, Serikali yake haitakubali uchochezi wa vurugu za kidini na kwamba, Serikali itawadhibiti.

Mambo mengine yaliyoibuliwa katika tathmini hiyo ni kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na haki msingi za binadamu, hasa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kutokana na imani za kishirikina na uroho wa utajiri wa haraka haraka.All the contents on this site are copyrighted ©.