2013-01-29 14:29:57

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani iwe ni fursa makini ya kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya mwanadamu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, linawaalika waamini kumwilisha ndani mwao fadhila za kikristo zinazojikita katika haki, upendo na mshikamano wa dhati, kama kielelezo makini cha kujibu changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi. Hii ni nchi ambayo licha ya kuwa na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali, imeendelea kujivunia utajiri wa maisha ya kiroho pamoja na utamaduni wa amani na utulivu, kila mtu akiheshimiwa na kuthaminiwa na Jamii husika.

Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand linawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; walinde na kutunza mazingira, ili dunia iendelee kuwa ni mahali paguri zaidi pa kuishi sanjari na kuondokana na ubinafsi unaoendelea kushika kasi miongoni mwa Jamii, kwa watu kukumbatia mno malimwengu na kusahau Mapokeo na tamaduni njema za nchi yao.

Kuna haja kwa Jamii kuendelea kuwekeza katika elimu ya utunzaji bora wa mazingira, sanjari na kukuza utamaduni wa upendo na mshikamano wa dhati, mambo ambayo yanaendelea kumong’onyoka siku hadi siku katika ulimwengu wa utandawazi. Kwenye miji mikubwa, ubinafsi unaonekana kuwa kama ndio mtindo wamaisha, kila mtu anajitafuta mwenyewe na wala maisha ya jirani yake, hayamgusi kamwe.

Ubinafsi unaanza kukomaa, kiasi kwamba, ni vigumu kwa sasa kuweza kufanya mabadiliko ya dhati. Mwaka wa Imani, iwe ni changamoto kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuwekeza katika fadhila za Kikristo.

Watu wamekuwa ni watumwa wa matangazo ya biashara na mitandao ya mawasiliano ya Jamii, mambo yanayoleta athari kubwa hata katika maisha ya familia. Watu wanatumia muda mrefu kuzungumza kwenye simu, kuperuzi kwenye mitandao na pengine hata kukosa nafasi ya kuzungumza ndani ya familia, hali ambayo inaweza kuleta madhara makubwa katika malezi na makuzi ya watoto pamoja na mahusiano ndani ya Familia.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya labari yasaidie kukuza na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia na kamwe yasiwe ni kikwazo cha heshima, utu na maadili mema. Matumizi ya mitandao ya Jamii yamekuwa kwa familia nyingi chanzo cha kinzani na mitigano; hatari kubwa inayoweza kuporomosha misingi bora ya ndoa na maisha ya kifamilia.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanayokwenda sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican iwe ni fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kujichotea utajiri mkubwa, uliobainishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa, Neno la Mungu, Nafasi na dhamana ya waamini walei katika kuyatakatifuza malimwengu bila kusahau majadiliano ya kidini na kiekumene, kama njia muafaka ya Uinjilishaji Mpya, iliyobainishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ikatiliwa mkazo na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya.

Miaka ishirini tangu kuchapishwa kwa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, iwe ni fursa kwa waamini kufahamu kwa kina Imani ambayo Mama Kanisa anaiungama, anaiadhimisha, anajitahidi kuimwilisha na kuisali. Waamini wajibidishe kuyafahamu Mafundisho tanzu ya Kanisa bila kusahau umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, kanuni na mwongozo kwa waamini walei katika mchakato unaopania kuyatakatifuza malimwengu.

Mwaka wa Imani, wanasema Maaskofu, ujenge na kuimarisha Injili ya Upendo inayomwilisha Imani katika matendo, kwa kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kila mtu aweze kutambua heshima na utu wake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kuna umati mkubwa wa wagonjwa, wazee, vijana na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, bila kuwasahau wale ambao wanakabiliwa kutolewa mimba kutokana na utamaduni wa kifo; wote hawa wana njaa na kiu ya Injili ya Upendo. Ni mwaliko kwa waamini kuyatumia malimwengu kwa busara kwa ajili ya mafao ya wengi na maendeleo endelevu ya binadamu, wawe mstari wa mbele kuyatakatifuza malimwengu, kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu.

Familia za Kikristo ziwe ni daraja linalounganisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, kiutu na kimaadili, kwa kutambua kwamba, Familia ni shule ya kwanza ya maisha ya binadamu, kumbe wazazi wana wajibu mkubwa katika malezi na majiundo ya watoto wao. Familia ni shule ya haki, amani na upendo unaopaswa kujionesha katika Jamii; ziwe ni chachu ya ujenzi wa mshikamano wa upendo na udugu, ili kweli amani iweze kutawala katika mioyo na maisha ya watu.








All the contents on this site are copyrighted ©.