2013-01-29 10:38:29

Elimu inayokumbatia utamaduni wa maisha ni muhimu katika mchakato wa kukabiliana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya wanawake!


Baraza la Maaskofu Katoliki India linasema kwamba, ili kupambana fika na vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa wanawake, kuna haja kwa Jamii kuwekeza katika elimu bora, itakayowawezesha wananchi kutambua na kuheshimu utu wa kila mtu.

Akizungumzia kuhusu tatizo la unyanyasaji wa wanawake nchini India, Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India anasema, kuna haja ya watu kutambua kwamba, kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, jambo linalompatia utu na heshima yake kama binadamu ndani ya Jamii, licha ya makando kando mengine yanayoweza kujionesha katika Jamii. Ikiwa kama watu wataiona na kuheshimu ile sura na mfano wa Mungu kati yao, vitendo vya unyanyasaji na dhuluma kwa wanawake nchini India vitakwisha.

Unyanyasaji wa wanawake unajionesha pia katika utamaduni unaokumbatia kifo kwa kuwalazimisha kutoa mimba; mauaji ya watoto wachanga, ambao wakati mwingine wanatupwa kwenye mapipa ya taka kana kwamba, si binadamu! Wanawake wanabaguliwa na wakati mwingine wanakabiliana na nyanyaso ndani ya Familia zao. Matukio yote haya anasema Kardinali Gracias yanaacha kurasa chungu katika maisha ya wanawake nchini India na sehemu nyingine za dunia. Watu watambue na kuheshimu utakatifu wa maisha pamoja na kuenzi haki msingi za binadamu.

Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa kwa vijana inawajengea uwezo wa kuthamini na kuenzi utamaduni wa uhai. Hii ni dhamana inayoendelezwa na Mama Kanisa katika kulinda na kutetea utu na heshima ya kila mtu. Siku ya usawa kwa wote nchini India, iliyoadhimishwa Jumapili iliyopita imekuwa ni fursa nyingine kwa Jamii kuhakikisha kwamba, inatoa kipaumbele kwa heshima, utu na haki msingi za wanawake, ili waweze kutekeleza majukumu yao ndani ya Jamii na Kanisa kwa ujumla.All the contents on this site are copyrighted ©.