Barua ya kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, 2013
Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia hivi karibuni limehitimisha mkutano wake mkuu uliokuwa
unaongozwa na kauli mbiu "Bwana anataka nini kwako? ila kutenda haki, na kupenda rehema,
na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako". Imekuwa ni fursa ya kuangalia hali halisi
ya nchi ya Zambia kwa kumshukuru Mungu kwa mema na ukarimu wake; daima wakitembea
katika njia ya upendo, haki na huruma, ukweli na upendo.
Maaskofu katika ujumbe
wao wanapembua kwa kina na mapana hali ya kisiasa nchini humo tangu walipoamua kufuata
mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, kunako mwaka 1991. Wananchi wa Zambia walitamani
kuwa na uhuru mpana zaidi kwa kukumbatia mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, lakini
matumaini haya bado hayajafikiwa kutokana na kinzani zinazoendelea kujitokeza miongoni
mwa Vyama vya Kisiasa, hali inayoonekana kwamba, wanasiasa wengi wana uchu wa madaraka
na wanaoumia ni wananchi wa kawaida.
Maaskofu wanawaomba wanasiasa nchini
Zambia kuonesha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia, utu na heshima wanapotekeleza
wajibu na dhamana yao katika Jukwaa la Kisiasa; daima wakitafuta mafao ya wengi na
maboresho ya maisha ya maskini.Wanatoa mwaliko kwa Tume ya Uchaguzi Zambia kuhakikisha
kwamba, inapanga na kuendesha chaguzi ndogo ili wananchi waendelee kuwa na wawakilishi
katika maeneo husika. Hapa kila mtu anapaswa kutekeleza wajibu wake kikamilifu. Ni
matumaini ya Maaskofu Katoliki Zambia kwamba, Katiba Mpya itaweza kutoa mwongozo maalum
utakaoratibu chaguzi ndogo.
Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, kuna baadhi
ya wanasiasa wanajitafuta wenyewe na wako katika Jukwaa la kisiasa kwa ajili ya mafao
yao binafsi, ndiyo maana wako tayari kuhama kutoka chama kimoja hadi kingine, ili
kutafuta masilahi. Umefika wakati kwa wanasiasa kujitathmini na kujijengea jina kwa
kuwa ni wanasiasa makini, waaminifu na wa kweli katika misingi wanayopigania wakiongozwa
na dhamiri nyofu kwa ajili ya mafao ya Jamii.
Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia
linalipongeza Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu yake. Lakini bado kuna
malalamiko makubwa ya matumizi mabaya ya madaraka ya umma dhidi ya vyama vya upinzani
na vyama vya kiraia vinapotaka kufanya shughuli zao.
Jeshi la Zambia linapaswa
kuzingatia maadili, kanuni na weledi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kulinda
na kusimamia sheria na utulivu bila ubaguzi wala upendeleo kwa Chama Tawala. Wanaitaka
Serikali ya Zambia kutekeleza demokrasi kabla ya nchi haijatumbukizwa katika maafa,
kwa kulinda na kudumisha ulinzi na usalama.
Maaskofu pia katika barua yao ya
kichungaji wanaliangalia tatizo la Barotseland, sehemu ambayo bado kuna uvunjifu mkubwa
wa haki msingi za binadamu, hali ambayo kamwe haiwezi kukubaliwa na kwamba, inapaswa
kusitishwa mara moja. Serikali ijenge mazingira ya kirafiki ili kuweza kupata ufumbuzi
wa kudumu wa mgogoro huu, daima wakijitahidi kujenga na kudumisha majadiliano ya kweli
bila vitisho.
Katiba ya Zambia inawahakikishia wananchi wote wa Zambia haki
zao msingi; haki ya kuishi, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kujiunga na vyama pamoja
na makundi mbali mbali bila kusahau uhuru wa dhamiri. Ni wajibu wa Serikali kulinda
na kutetea haki hizi msingi kwa raia wake, kwani kwa sasa hali inazidi kuwa mbaya
zaidi siku hadi siku. Serikali imekuwa ikitumia nguvu, vitisho pamoja na kuwatia mbaroni
wanasiasa na raia wanaoonekana kuipinga Serikali. Maaskofu wanasema, Serikali inapaswa
kuheshimu haki msingi za binadamu.
Mahakama ni kati ya mihimili mikuu mitatu
ya dola inayopaswa kutekeleza majukumu yake kwa uhuru bila ya kuingiliwa. Kadiri siku
zinazovidi kuyoyoma watu wanaanza kukosa imani na Mahakama. Wananchi wa Zambia wanasubiri
kwa hamu mabadiliko makubwa ya Mahakama pamoja na kutaka utata unaoendelea kujionesha
katika masuala ya Mahakama kupewa ufumbuzi wa haraka.
Ni matumaini ya Baraza
la Maaskofu Katoliki Zambia kwamba, Muswada wa Katiba Mpya ya Zambia utaendelezwa,
ili hatimaye, wananchi waweze kuwa na Katiba Mpya. Ili kufikia lengo hili, Serikali
haina budi kutenga bajeti kwa ajili ya jukumu hili, ili hatimaye, wananchi waweze
kupigia Muswada huu kura ya maoni kama wana ukubali au wana ukataa. Serikali katika
maamuzi mengi imejikuta ikiyafanya peke yake kiasi cha kukosa uongozi shirikishi ambao
ni muhimu sana katika kukuza na kuimarisha demokrasia.
Serikali badala ya
kujenga utamaduni wa majadiliano na wadau mbali mbali, imejikita ikitoa matamko, kama
ilivyofanya katika Sekta ya Elimu: uhusiano kati ya Serikali na Kanisa. Hapa kulihitajika
majadiliano ya kina, ili kuweza kufikia uamuzi mzuri zaidi. Pamoja na mambo mengine,
Maaskofu Katoliki Zambia wanasema, kuna haja ya Serikali kupitia Mamlaka ya habari
na Teknolojia ya Mawasiliano Zambia (ZICTA) kusajili namba zote za Simu ili kudhibiti
vitendo vya uharifu vinavyozidi kuongezeka kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano.