Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha
na utume wa Kanisa
Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika hotuba
yake ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumatatu tarehe
28 Januari 2013 anasema kwamba, mkutano huu unafanyika wakati ambapo Maaskofu Katoliki
Italia wanafanya hija ya kitume mjini Vatican sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Maaskofu wanamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kutambua
ushuhuda uliotolewa na Papa Paulo wa Sita na sasa anaweza kutangazwa kuwa Mwenyeheri.
Maaskofu
wako katika hija ya matumaini inayowawajibisha kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa
na kufufuka kutoka katika wafu bila kikomo na kwamba, hii ndiyo hoja wanayotaka kuifanyia
kazi katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ili kuwasaidia watu wanaoogelea katika
utupu wa jangwa na maisha ya kiroho na kimaadili kuonja ile furaha ya kuwa mfuasi
wa Kristo, kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Idadi
ya Wakristo waliouwawa kikatili sehemu mbali mbali za duniani kwa mwaka 2012 inatisha
kutokana na kuibuka kwa watu wenye misimamo mikali ya kidini, utaifa pamoja na uchu
wa madaraka kama ilivyotokea: Nigeria, Kenya, DRC na Mali. Kinzani za kikabila na
kijamii ni kati ya mambo yanayoendelea kuvunja misingi ya haki, amani na utulivu.
Kardinali Bagnasco anasema kwamba, baa la njaa linaendelea kutesa mamillioni
ya watu kuliko hata ilivyo kwa athari za myumbo wa uchumi kimataifa, changamoto ya
kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo unaosimikwa katika kanuni ya auni. Deni
kubwa la taifa na matumizi makubwa ya Serikali ni mambo ambayo yanapelekea ugumu wa
maisha na umaskini miongoni mwa wananchi wengi wa Italia.
Hali hii imepelekea
pia ongezeko la vijana wasiokuwa na fursa za ajira pamoja na umaskini wa kipato na
kihali kwa familia nyingi nchini Italia. Ni wajibu wa wanasiasa kuibua mbinu mkakati
utakaoiwezesha Jamii kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayoendelea kukatisha tamaa
pamoja na kukwamisha mchakato wa maendeleo. Sera na mikakati ya maendeleo haina budi
kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili.
Kanisa kwa upande wake, litaendelea kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa kutangaza Injili ya Upendo;
utunzaji bora wa mazingira pamoja na kutolea ushuhuda kweli za Kiinjili zinazobubujika
kutoka katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Liturujia ya Kanisa
iwe ni shule ya kusikiliza kwa makini Neno la Mungu pamoja na kukuza Ibada mbali mbali
zinazorutubisha maisha ya kiroho. Yote haya yanaweza kutekelezwa barabara ikiwa kama
Familia itakuwa imeshikamana kwa dhati na kwamba, msingi mkuu ni upendo wa dhati!
Kanisa litaendelea kutekeleza wajibu na dhamana yake katika Jamii na wala halina mpango
wa kuingilia masuala ya kisiasa, lakini, litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea
haki msingi za binadamu, mafao ya wengi pamoja na maisha bora kwa wananchi wengi.
Ni mwaliko kwa wananchi pia kutekeleza wajibu wao wa kisiasa kwa kushiriki
kikamilifu katika mchakato wa kupiga kura ili kuwapata viongozi bora watakaoliongoza
taifa kwa uzalendo, hekima na unyofu wa moyo, daima wakitafuta mafao ya wengi na wala
siasa lisiwe ni Jukwaa la kutafuta kujitajirisha! Zawadi ya maisha haina budi kulindwa
na kutetewa tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi anapofikwa na mauti ya kawaida
kadiri ya mpango wa Mungu.
Ni mwaliko kwa Jamii kujenga utamaduni wa uhai
kama njia ya kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa na wala si kwa kukumbatia
utamaduni wa kifo! Tunu bora za maisha ya Ndoa na Familia hazina budi kulindwa kama
mhimili mkuu wa maisha ya Kijamii unaojengeka katika upendo wa dhati, kwani mahali
ambapo kuna upendo wa kweli, anasema Kardinali Bagnasco, hapo Mungu yupo! Ndoa inajengeka
katika uhusiano kati ya Bwana na Bibi na matunda ya ndoa ni watoto ambao wana haki
ya kupata malezi ya wazazi wao. Maaskofu Katoliki Italia wanapinga ndoa za watu wa
jinsia moja!