2013-01-28 08:03:04

Utajiri wa nchi ni kwa mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kuwaneemesha wajanja wachache!


Askofu Michele Russo wa Jimbo Katoliki Doba, nchini Chad, aliyekuwa amefukuzwa nchini humo kutokana na tuhuma kwamba, mahubiri yake kuhusu matumizi ya rasilimali na utajiri wa nchi ya Chad ulikuwa unatumiwa vibaya kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache ameruhusiwa tena kurudi Jimboni mwake na kuendelea na shughuli zake za kichungaji kama kawaida. RealAudioMP3

Askofu Russo anasema, kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano ili kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, daima wakilenga kwa ajili ya kutetea mafao ya wengi. Kanisa Katoliki nchini Chad, liko mstari wa mbele ili kuhakikisha kwamba, linaendeleza dhamana ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu Russo anapanga kukutana na viongozi wa Serikali ya Chad ili kufafanua kuhusu mahubiri yake na jinsi ambavyo yalivyotafsiriwa kinyume na kusababisha yeye kufukuzwa nchini Chad, hatua ambayo ilipingwa na Kanisa. Anasema, kuna haja kwa viongozi wa Serikali waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali na utajiri wan chi ya Chad, kuhakikisha kwamba, wanatumia mapato ya utajiri huu kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wananchi wa Chad na kamwe usiwe ni kwa ajili ya mafao ya watu wachache ndani ya Jamii, wakati ambapo kuna umati mkubwa wa watu wanaendelea kutopea katika dimbwi la umaskini wa kipato, magonjwa na ujinga.

Idadi ya wananchi wa Chad kwa sasa inafikia million ishirini. Mapato ya nishati ya mafuta, yakitumiwa vyema kwa kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya wananchi, kwa hakika miundo mbinu ya barabara, shule na hospitali zitaweza kuboreshwa zaidi. Ni jukumu la viongozi wa Serikali kuhakikisha kwamba, Makampuni yanayo chimba mafuta yanalipa kodi inayostahili, ili iweze kutumika kwa ajili ya mafao ya wengi. Lakini, ikiwa kama viongozi wenyewe watakuwa wa kwanza kukumbatia rushwa na ufisadi, itakuwa ni vigumu sana wananchi wengi kupata maendeleo na hivyo kuondokana na umaskini, ujinga na maradhi.

Askofu Michele Russo anasema kwamba, Kanisa lina matumaini makubwa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, litaendelea kutekeleza wajibu wake wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu, kama kielelezo makini cha kumwilisha Imani katika matendo.

Anasema, anaipenda nchi ya Chad na kuwaheshimu watu wake na anatumaini kwamba, wataendelea kushikamana katika ujenzi wa matumaini ya Chad iliyo nzuri zaidi, inayoheshimu uhuru wa mtu kujieleza bila kumfunga kwa vitisho. Kanisa litaendelea kutekeleza wajibu wake wa kutoa huduma kwa wote bila ubaguzi wala uchoyo, kwani hii ni sehemu ya vinasaba vya utamaduni wa upendo na mshikamano unaojichimbia katika kanuni ya auni.
All the contents on this site are copyrighted ©.