Mshikamano wa Kanisa na wote wanaoteseka Mashariki ya Kati kutokana na vita na kinzani
za kijamii!
Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem, katika kipindi hiki cha taabu, mateso na mahangaiko
ya wananchi wengi wa Syria kutokana na vita na kinzani za kijamii zinazoendelea kujitokeza
nchini humo ameamua kuwaandikia waamini na wahudumu wote kwa kutambua mchango wao
katika kuwahudumia waathirika wa vita nchini Syria na kwamba, yuko pamoja nao kwa
njia ya sala. Uwepo wao ni kielelezo makini cha ushuhuda wa upendo na udugu miongoni
mwa Jamiiiliyosambaratika kutoka na vita. Anatambua na kuguswa na mahangaiko ya
wananchi wa Syria wakati huu wanapoendelea kufanya hija ya Njia ya Msalaba, wakishiriki
mateso ya Kristo yanayokoa; anapenda kutoa sala zake kwa wote waliotangulia mbele
ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko; wagonjwa wanaoteseka kutokana na kukosekana
kwa huduma, wale wanaokimbia ili kusalimisha maisha yao bila kuwasahau wale ambao
wameamua kubaki nchini mwao, licha ya mtutu wa bunduki kuendelea kurindima katika
mitaa na viunga miji yao. Haya ni mahangaiko na mateso ambayo Patriaki Twal ameyashuhudia
mwenyewe wakati alipofanya hija yake ya kichungaji kule Mafraq, Kaskazini mwa Mto
Yordani. Watu wenye mapenzi mema wanaendelea kujiuliza, Je, mateso na mahangaiko ya
watu hawa yataendelea hadi lini? Jambo linalosikitisha ni kuona kwamba, katika taabu
na mahangaiko haya, hawana lolote lile ambalo wanaweza kutekeleza ili kuokoa maisha
ya watu na kusitisha vita, kinzani na mgogoro unaoendelea nchini Syria. Patriaki
Twal anasema, anapenda kuunganisha sauti yake na wapenda amani kutoka pande mbali
mbali za dunia, kukazia umuhimu wa mshikamano wa upendo na udugu miongoni mwa wananchi
wa Syria, kama anavyoendelea kukazia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Kama
viongozi wa Kanisa wanaungana na waamini wote ili kuombea amani ili watu waweze kusitisha
kinzani na vita vinavyoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia
na badala yake, kuonesha ujasiri wa kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kweli, ili
hatimaye, amani, upendo na mshikamano kati ya watu viweze kushamiri katika mioyo yao!