2013-01-28 07:56:50

Maaskofu Katoliki Italia waanza mkutano wao


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 31 Januari 2013 linafanya mkutano wake, utakaojadili pamoja na mambo mengine kuhusu mabadiliko yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuhusu Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kwa kuzingatia kwamba, huduma ya upendo ni sehemu ya asili na vinasaba vya Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Mkutano huu utakuwa chini ya Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Maaskofu wanajadili na hatimaye, kupitisha Angalisho la shughuli za kichungaji, kwa kutambua umuhimu wake katika utume wa Kanisa unaojikita katika utajiri mkubwa wa Mama Kanisa kwa karne nyingi, lakini, unaopaswa kuangaliwa kwa mapana kwa kusoma alama za nyakati mintarafu mahitaji ya sasa.

Mkazo ni kuendelea kukazia umuhimu wa Katekesi kama njia makini ya kurithisha Imani ya Kanisa kwa waamini wanaoendelea na hija ya maisha yao hapa duniani, bila kusahau umuhimu wa majiundo makini na ya kina kwa Makatekista wanaopewa dhamana ya ya kurithisha Imani ya Kanisa kwa Wakatekumeni na vijana wa kizazi kipya. Makatekista wasipokuwa makini, Kanisa linaweza kujikuta likiwa na waamini hoi bin taabani, wasioweza kukiri, kuadhimisha, kuiishi, kusali na kuimwilisha Imani yao katika matendo.

All the contents on this site are copyrighted ©.