2013-01-28 09:17:16

Kumbukumbu ya madhulumu dhidi ya Wayahudi ni onyo kwa kila mtu, ili mauaji kama haya yasijirudie tena!


Tarehe 27 Januari 2013, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliungana na Jumuiya ya Kimataifa kuwakumbuka wote waliopoteza maisha yao kutokana na madhulumu yaliyofanywa na utawala wa Kinazi dhidi ya Wayahudi. Kumbu kumbu hii anasema Baba Mtakatifu inapaswa kuwa ni onyo kwa kila mtu, ili madhulumu na mauaji ya kinyama yaliyotjitokeza wakati ule yasijirudie tena. RealAudioMP3

Ni changamoto kwa kila mtu kuondokana na vitendo vya chuki na ubaguzi na badala yake, watu wajenge utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana, wakisimama kidete kulinda na kutetea utu wa kila mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Jumuiya ya Kimataifa, Jumapili iliyopita imeadhimisha pia Siku ya 60 ya Wagonjwa wa Ukoma Duniani. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anapenda kuendelea kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wagonjwa wa Ukoma sehemu mbali mbali za dunia. Anawatia moyo watafiti, wafanyakazi wa sekta ya afya; wanachama wa vyama vya kitume kwa ajili ya wagonjwa wa Ukoma na kwa namna ya pekee wanachama wa Chama cha Marafiki wa Wagonjwa wa Ukoma cha Raoul Follereau.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaweka wagonjwa wote wa Ukoma chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Damiano De Veuster na Mtakatifu Marianna Cope ambao waliyamimina maisha yao kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Ukoma.

Baba Mtakatifu pia aliungana na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa wanaombea amani katika nchi Takatifu na wote waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu pia alimkumbuka Hayati Kardinali Jozef Glemp aliyefariki dunia hivi karibuni. Anamshukuru Mungu kwa maisha na utume wa Kardinali Glemp, anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kumkirimia maisha ya uzima wa milele.









All the contents on this site are copyrighted ©.