2013-01-26 09:04:17

Wafrancisan wako mjini Assis kushiriki katika Mkutano mkuu wa 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika!


Watawa wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francis wa Assis kutoka nchi sitini na tano, wanaendelea na mkutano mkuu uliofunguliwa hivi karibuni na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 17 Februari 2013. Mkutano mkuu ni kipindi cha sala, tafakari pamoja na upembuzi yakinifu utakaoliwezesha Shirika kujiwekea mikakati ya maisha na shughuli za kichungaji kwa siku za usoni.

Ni fursa kwa Wafranciscani kujichotea nguvu na ari mpya ya maisha ya kiroho tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo kwa kukazia kwa namna ya pekee Uinjilishaji Mpya, changamoto inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia

Huu ni mkutano mkuu wa mia mbili, tangu Shirika hili lilipoanzishwa na Mtakatifu Francisco wa Assisi na unafanyika kila baada ya miaka sita, ili kumchagua mkuu wa Shirika pamoja na Wajumbe wa Halmashauri kuu ya Shirika. Idadi ya Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francis wa Assisi inaendelea kuongezeka maradufu Barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini, wakati ambapo miito ya Shirika kwa upande wa Bara la Ulaya na Amerika inazidi kuchechemea kwa kasi ya ajabu.
All the contents on this site are copyrighted ©.