2013-01-26 07:42:11

Maoni ya Wasomi kutoka Roma kuhusu Katiba Mpya ya Tanzania


Mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya ya Tanzania unaendelea vyema, awamu ya kwanza ilikuwa ni kuhamasisha na kukusanya maoni kutoka kwa watanzania mmoja mmoja. Hatua ya pili imekuwa ni kukusanya maoni kwa makundi maalum. Yafuatayo ni baadhi ya maoni yaliyotolewa na wanafunzi wanaosoma mjini Roma, kama sehemu ya mchango wao katika kuandika Katiba Mpya ya Tanzania.
1. Kuhusu Mahakama ya Kadhi:
Mahakama hii ni ya kidini na inahusiana na utatuzi wa maswala ya kidini. Hivyo basi, kutokana na kwamba Tanzania yetu tangu kupata uhuru wake inajukana kama nchi isiyo fuata misingi ya dini yoyote, swala la Mahakama ya Kadhi isiingie kwenye katiba; mahakama iendelee kubaki kama mmojawapo wa mihimili mikuu ya nchi inayo ratibu maswala ya dini husika, bila kuihusisha Katiba ya nchi ambayo ni ya wananchi wote wafuasi wa dini fulani na wasio fuata dini yoyote. Mahakama za kidini zisiingie katika katiba kwani Tanzania haina dini.
2. Kuhusu Tanzania kujiunga na OIC
Jumuiya ya Nchi za Kiislam OIC ina malengo na itikadi zake zinazojikita hasa katika masuala ya kidini. Tanzania hadi sasa haina dini yoyote rasmi ila ni wananchi wake wanao abudu kwenye dini na madhehebu mbalimbali. Ikiwa kuna wananchi wanaotaka kujiunga na Jumuiya hii wapewe nafasi kama watu binafsi na si kama nchi. Tanzania isijiunge na OIC kwa kuwa hii ni Jumuiya ya Kidini. Suala la Tanzania kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Vatican halina uhusiano wowote na madai ya baadhi ya watu kutaka Tanzania kujiunga na OIC.
3. Kuhusu mfumo wa Elimu
Kwakuwa Serikali inalo jukumu la kuhakikishia wananchi wake Elimu, mfumo wa Elimu usiwe wa kidini badala yake uendelee kusimamiwa na serikali itakayokuwa madarakani.Mchango wa dini mbalimbali katika sekta hii uendelee kuheshimiwa na kuthaminiwa, ila serikali iliyoko madarakani ndiyo itoe taratibu na sheria (zisizoshikamana na dini yoyote) zinazopaswa kufuatwa katika swala zima la utoaji Elimu.
4. Kuhusu uteuzi wa viongozi wa serikali na wa mashirika ya kiserikali
Uteuzi wa viongozi hawa uzingatie sifa za anayeteuliwa na wala usifanyike kulingana na sera za kiundugu au kidini. Si kwa sababu mteuliwa ni rafiki au ndugu wa Kiongozi fulani au ni muumini wa dini fulani, basi anafaa kushika madaraka. Nyadhifa zitolewe kwa kuzingatia “Mastahili, sifa na vigezo vinavyohitajika.
5. Kuhusu uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Hadi sasa watanzania tunajua kuwa bara na visiwani ni Taifa moja na kwamba hatuna tofauti yoyote kama raia. Hivyo basi, kwakuwa Zanzibar na Tanzania bara ni nchi moja, Raisi wa Jamhuri ya Muungano atoke upande wowote ule wa Muungano na kusiwepo utaratibu wa kupata Rais kwa zamu kati ya Tanzania bara na Zanzibar. Utaratibu wa kupata Rais kwa zamu kati ya pande hizo mbili unaweza ukawa hatari na kutishia zaidi usalama na amani ya Taifa kwani inawezekana kutokea kwamba kusitokee aidha mgombea nafasi hiyo mahali ambapo Rais alitakiwa kutokwa kadiri ya mfuno uliopo hadi sasa.
Nafafanua: ikiwa kwa mfano kwenye uchaguzi ujao Rais anapaswa kutokea Zanzibar au bara, na ikatokea kwamba kwenye ukanda huo hakuna mgombea aliyejitokeza, au aliyejitokeza asipigiwe kura, nini kitafanyika? Kumbe kipengele kinachosititza kuwa Rais achaguliwe kwa kuzingatia bara na visiwani kingeweza kuangaliwa upya na kufanyiwa marekebisho ili Rais achaguliwe kutoka eneo lolote la Tanzania.
6. Kuhusu utoaji mimba
Utoaji mimba ni swala linalohusu haki msingi za binadamu zinazoongozwa na dhamiri nyofu. Hakuna serikali yoyote inayoweza kuingilia dhamira ya mwananchi. Kama vile ambavyo serikali haiwezi kumchagulia mwananchi yeyote mwenza wa maisha, au kuwaamuru wananchi kuvaa mavazi yaliyoshonwa kwa mtindo fulani au ya rangi fulani, hali kadhalika, serikali haipaswi kujiingiza kwenye maswala ya kuratibu na kuhalalisha kisheria maswala yanayohusu dhamira na hasa mauaji ya watu wasio kuwa na hatia!
Jukumu la serikali ni kulinda maisha na usalama wa raia wake wote na si kuratibu mauaji ya baadhi ya raia ambao bado hawajazaliwa. Licha ya hilo, mila na desturi za kiafrika si mila za mauaji bali ni mila zinazotetea uhai na kuulinda. Utoaji mimba ni utamaduni wa kifo usiopaswa kukumbatiwa na mwanadamu yeyote na hasa chombo kinacho ratibu maisha ya wananchi kama ilivyo Katiba ya nchi. Katiba ilinde haki za watoto ambao bado hawajazaliwa.
7. Kuhusu ndoa za watu wa jinsia moja
Serikali isitambue ndoa ya watu wa jinsia moja na kuiweka katika Katiba ya nchi, kwa kuwa ni jambo linalo kwenda kinyume na maadili ya kiutu na kijamii. Hivyo swala hili lisipate nafasi katika Katiba ya nchi. Kama ilivyo hoja iliyopita, hata hii inayofuata inahusu dhamira ya mtu binafsi. Kama baadhi ya wananchi wakiamua kuishi muunganiko (kwani haiwezi kuitwa ndoa) wa watu wa jinsia moja, liwe ni chaguo lao binafsi, ila lisitambulike kikatiba! Katiba ya nchi izingatie maadili na utu wema.
8. Uraia wa nchi mbili:
Kuna haja kwa Katiba ya Tanzania kusoma alama za nyakati kwa kuruhusu raia wake kuwa na fursa ya uraia wa nchi mbili pale inapowezekana ili kuweza kufaidi matunda ya jasho la watanzania wanaoishi ughaibuni.
All the contents on this site are copyrighted ©.