2013-01-25 07:48:09

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Ni mara nyingine tena katika utaratibu wa kawaida wa tafakari Neno la Mungu tunapokutana katika mtandao kushirikishana tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya III ya mwaka C. RealAudioMP3

Katika tafakari yetu tunamwona Mtume Paulo akiendelea kukazia fundisho lake la kuwa sisi sote chimbuko letu ni Kristo. Tuko tofauti kwa maana ya kuwa wengine ni Wayahudi, wengine ni Wayunani na hata wengine kwa sababu ya dhuluma wamekuwa watumwa. Lakini anasema, akisha kuja Kristo hakuna tena matabaka haya bali umoja kamili katika mwili mmoja ulio na viungo vingi.

Anatangaza uzuri wa utofauti ulio katika kufaidiana. Anajiuliza, hivi mwili wote ungekuwa jicho, kusikia kungetokeaje? Basi, kujivuna katika maisha ya kila siku kwa sababu ya mali au uwezo wa akili au kazi niliyonayo ni ukosefu wa maarifa na ustadi katika kufikiri. Kumbe udhanifu yakwamba wengine ni dhaifu ni chimbuko la mafarakano ambayo tunapaswa kuyaepuka kabisa.

Hata hivyo yafaa kukumbuka kuwa Kristo ameweka makundi maalumu ili Neno lake lisonge mbele. Mtume Paulo anasema wa kwanza ni Mitume ambao mahalifa wao ni Maaskofu, hawa ni nguzo za imani, yafaa kuwasikiliza na kushika mafundisho yao ambayo ni mafundisho ya Bwana. Wanafuata manabii na Walimu ambao hutangaza ujumbe wa Mungu na hatimaye miujiza, karama za kuponya na kunena lugha mbalimbali.

Katika Injili ya leo Mwinjili Luka anaanza Injili yake akionesha namna alivyoweza kuandika Injili, mbinu alizotumia kupata uhakika wa mambo, na tunapata kuona jina la mtu ambaye Injili inaelekezwa kwake yaani Teofilo Mtukufu. Jina Teofilo ni jina la Kigriki lenye kumaanisha “yule anayempenda Mungu”. Katika hili mara moja twaweza pia kufikiri toka jina hili kuwa Luka anaelekeza Injili yake kwa wale wanaompenda Mungu, wanaofanya utafiti wa kiroho na kichungaji kumjua Mungu. Watu hawa ni pamoja sisi taifa lake.

Bwana yuko Nazareti, amerudi nyumbani na siku ya Sabato anaingia katika Sinagogi na anasoma sehemu ya chuo cha Nabii Isaya, isemayo Roho wa Bwana yu juu yangu amenipaka mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Kisha kuweka chini chuo cha Isaya anatangaza tena mara ya pili kuwa sasa maneno haya yamekamilika katika yeye.

Bwana anajisalimisha kwa Roho wa Mungu ili aweze kufanya kazi ya kuokoa walio katika mashaka na matatizo mbali mbali ya maisha kama vile utumwa wa kiroho na kimwili na wanaoteswa kwa sababu ya imani yao. Kwa sababu daima Bwana wetu Yesu Kristo ametimiza kazi yake akimtegemea Baba yake tunaweza kusema bila kusahau kuwa yeye ndiye Mungu, ndiye Teofilo wa kweli ambaye Mt. Luka anaelekeza Injili yake.

Mpendwa, ni kwa namna gani nasi twaweza kushiriki kazi ya Teofilo kwa ajili ya taifa la Mungu? Twaweza kuishi ule upendo ambao Mungu anatuonjesha kila siku ya maisha yetu kwa njia ya Neno lake? Je, twatambua kuwa Kristo ni mjumbe wa Mungu wa Agano Jipya na ambaye kwa kutaka kusema nasi kwa uhakika amejifanya mtu na ni mwaminifu kwa Baba yake na hivi sisi tukialikwa kumfuata kila siku ya maisha yetu?

Tunaalikwa kila siku kutambua kuwa kumpenda Mungu ni kumtambua Kristo aliyefanyika mwili na akashiriki maisha yetu. Ni kukazia macho yetu kwake kama tulivyosikia katika Injili “waliokuwa katika Sinagogi wakamkazia macho” Bwana anawaonesha uhalisia wake yaani mtangazaji wa uhuru! Sisi Je, uhalisia wetu twautambua?

Tunapaswa kurudi katika ubatizo wetu na kutambua kuwa tumekuwa makuhani, wafalme na manabii! Wajibu wa vyeo hivi unaturudisha palepale kwa Bwana anapojionesha uhalisia wake, kuondoa dhuluma katika maisha ya watu, kwamba tunapaswa kutenda kama Bwana alivyotenda na anavyotaka daima.

Tunapomalizia tafakari hii tunarudi katika somo la kwanza tunapowaona Waisraeli wakirudi toka utumwani, Nabii Nehemia anahadithia jinsi walivyosikiliza Torati na kutoa machozi. Ndiyo kusema Neno la Bwana liliwaletea furaha mpaka wanafikia machozi ya furaha kama bibi arusi atoavyo machozi anapoenda kuolewa. Ndiyo kusema Neno la Mungu limewaingia na kulisikiliza kwa makini.

Tunaweza kusema Wana wa Israeli wanaporudi wanafanya Agano na Mungu na wanahaidi kumhimidi Mungu katika maisha yao. Tunaona Ezra analeta Torati mbele ya kusanyiko la watu, Wake kwa Wanaume anasimama juu ya Mimbari na anatangaza ukuu wa MUNGU na kumhimidi Bwana. Watu wanaitika na kusema amina, amina na kuinua mikono yao na kisha kuinamisha vichwa vyao na kumsujudu Bwana kifudifudi.

Naye Nehemia alikuwa mmoja wa waliowafundisha watu na kuwaambia watu wote kuwa siku hii ni takatifu kwa Bwana, msilie kamwe, maana walilia waliposikia maneno ya Torati. Kuleni na kunywa kilichonona na kisha mpelekeeni yule asiyewekewa, siku hii ni takatifu na furaha ya Bwana ni nguvu zenu. Kumbe baada ya kuelewa Neno la Mungu na kutoa machozi ya furaha kadiri ya Nabii tunapaswa kwenda kutangaza habari njema. Bwana katika Agano Jipya anatutuma akisema Enendeni duniani kote mkatangaze habari njema. Mt. 28:19-20.

Neno la Mungu ni taa ya maisha yangu uwe ndiyo wimbo wako wa kila siku lakini hasa kuliweka katika matendo ukilitangaza kwa mataifa. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.


All the contents on this site are copyrighted ©.