2013-01-25 14:02:51

Papa anaungana na watetezi wa zawadi ya uhai kwa njia ya Twitter katika maandamano nchini Marekani


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amewaandikia waandamaji wote wanaoshiriki katika maandamano ya kutetea zawadi ya uhai nchini Marekani, akiwahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala na kwamba, anawaombea wanasiasa wote watakaosimama kidete kutetea watoto ambao hawajazaliwa pamoja na kudumisha utamaduni wa uhai.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu unafanya rejea kwenye maandamano ya kutetea zawadi ya uhai, tukio ambalo linafanyika kila mwaka ifikapo tarehe 25 Januari kwa kuwashirikisha wanaharakati wanaoendelea kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Itakumbukwa kwamba, ni tukio linaloungwa mkono pia na Kanisa Katoliki nchini Marekani. Kwa mara ya kwanza tukio hili lilifanyika kunako mwaka 1973 kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama kuu ya Marekani kuruhusu utoaji mimba.

Baba Mtakatifu anaendelea kujimwaga katika matumizi ya mitandao ya kijamii kwa njia ya ujumbe mfupi, kama sehemu ya mkakati wake wa kuinjilisha hata mitandao hii ili iweze kuwa ni jukwaa la majadiliano ya tunu msingi za maisha na kweli za Kiinjili.All the contents on this site are copyrighted ©.