2013-01-25 09:24:39

Msikubali kukumbatia utamaduni wa kifo!


Shirika la Kikatoliki la Maisha na Familia nchini Canada, linapinga muswada uliopitishwa hivi karibuni nchini humo wa kutaka ipitishwe sheria itakayowaruhusu madaktari kuwasaidia watu kupata kifo laini au kwa lugha ya kitaalam, eutanasia. Shirika hili linaunga mkono jitihada za Serikali ya Canada kuhakikisha kwamba, wagonjwa walioko kufani wanapata tiba mahususi, kama heshima kwa utu wa mgonjwa, lakini wanapinga vikali madaktari kutoa msaada wa kitabibu kwa wagonjwa walioko kufani ili eti waweze kufa kwa heshima!

Vitendo vya namna hii ni kuvunja sheria, maadili ya kazi pamoja na athari nyingine zinazoweza kupatikana kutokana na utekelezaji wa muswada huu. Maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kulindwa na wala si jambo la kuchezea kadiri ya matakwa ya wanasiasa madarakani.

Tayari Shirika hili limekwisha wasilisha pingamizi la kisheria dhidi ya muswada huu kwani ni mauaji yanayotaka kuhalalishwa kwa njia ya sheria za nchi, kinyume kabisa cha Katiba inayotetea uhai wa mtu! Ukweli ni kwamba, hata katika nchi zile ambazo Eutanasia imekubalika kisheria kama Ubelgiji, lakini imekuwa ni vigumu sana kuweza kudhibiti vitendo vya madaktari katika kutoa uhai wa mwanadamu.

Muswada wa sheria wa kifo laini unatarajiwa kujadiliwa na Bunge la Canada Mwezi Juni, 2013. Lakini kwa watu wanaotaka kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, huu ni wakati wa kuchukua hatua ili kupinga vitendo kama hivi kwani hapa ni mauaji na wala hakuna huruma kwa wagonjwa wanaoteseka! Kama sheria hii itapitishwa, basi itakuwa ni sheria ya mauaji nchini Canada.

Waswahili wanasema, ukiona mwenzako ananyolewa, wewe anza kutia maji! Sheria hizi zinaanza safari yake mbali huko Ughaibuni, baada ya miaka michache zinaibuliwa pia katika Nchi Maskini duniani kama sehemu ya masharti ya kupata misaada!
All the contents on this site are copyrighted ©.