2013-01-25 08:27:26

Hatima ya mchakato wa Mabadiliko ya Katiba Tanzania 2013


Mchakato wa kutoa maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Tanzania unaendelea vyema kadiri ya wachunguzi wa masuala ya kisiasa. Baraza la Maaskofu Katoliki bado linaendelea kuwahamasisha waamini na watanzania wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika utoaji wa maoni kwa kuzingatia mafao ya wengi, umoja wa kitaifa, haki na amani. RealAudioMP3
Leo katika sehemu hii ya mwisho wa makala kuhusu maoni ya Katiba, Baraza la Maaskofu linaangalia kuhusu: Kubadili Katiba, mgombea binafsi, vyama vya kisiasa, muundo wa maeneo ya uwakilishi, ubunge na sifa zake; matokeo ya uchaguzi wa Rais, Baraza la Wazee na hatima ya Mchakato wa maoni ya Katiba mpya.
Kubadilisha Katiba
Iwe wazi kutoruhusu Bunge kurekebisha Katiba kadiri ya matakwa yao. Mabadiliko yafanyike kwa ridhaa ya wananchi. Hapa tunaweza kubainisha na kuainisha mambo ambayo hayawezi kuguswa kabisa na Bunge. Vipengele hivyo msingi katika Katiba vibadilishwe tu na wananchi kwa kura ya maoni. Vipengele vingine ambavyo siyo vya msingi viruhusiwe kubadilishwa na bunge kwa kura si chini ya theluthi mbili. (Ila hii itawezekana tu kama Katiba itawapa wananchi uwezo wa kuwawajibisha wabunge wao kwa kuwaondosha au “recall” wasiporidhika na uwakilishi wao).
Mgombea huru/ binafsi
Ni vema kuruhusu ili kuwezesha wale ambao hawapendi kujiunga na vyama waweze kuwa na haki ya kugombea nafasi za urais, ubunge na udiwani. Hii itasaidia pia viongozi hawa kuwajibika zaidi na kwa wananchi badala ya kujali zaidi maslahi ya chama kama ambavyo imeonekana. Itazuia chuki na uhasama ndani ya vyama kumwondoa mbunge ambaye ni chaguo la wananchi na wanampenda.
Vyama vya siasa
Ni muhimu sheria ya kuanzisha na kuendesha vyama vya siasa ishinikize vyama vyenye kukubalika na kuwakilisha wananchi kwa kuzingatia umoja wa Taifa na kupiga vita ubaguzi wa ukabila, dini au makundi mangine yoyote. Vilevile kuwe na vigezo vya vyama kukubalika na wananchi kwa kiasi cha upeo utakaokubalika. Na pia kuwe na mwongozo kuhusu matumizi na vyanzo vya mapato ya vyama vya siasa kwa ajili ya kudhibiti rushwa na kutekwa na matajiri.
Muundo wa maeneo ya uwakilishi
Maeneo haya: mikoa, wilaya na majimbo yagawanywe kwa kuzingatia vigezo wazi: idadi ya watu, ukubwa wa eneo na hata rasilimali zilizopo. Ugawaji wa bajeti uwe wa kuwezesha pia kuleta maendeleo kiuwiano kwa maeneo mbalimbali ya nchi ili kusiwe na tofauti kubwa ya maendeleo baina ya kanda au maeneo mbalimbali ya nchi. Wazo hili linakuwa wazi zaidi tunapoangalia mgawanyo baina ya Bara na Visiwani.
Kumwondoa mbunge madarakani kabla ya muda kuisha
Ili kuhimiza uwajibikaji kwa wananchi, Katiba iwape wananchi uwezo na utaratibu wa kumwondoa mbunge wao madarakani ikiwa wamethibitisha kuwa hawafai (kwa mfano kulingana na michango yake na kura zake Bungeni kama zina tija kwa wananchi anaowawakilisha).
Elimu na ukomo wa Ubunge
Kipindi cha ubunge kiwe na ukomo wa vipindi viwili, na pia nafasi hiyo igombewe na wenye elimu isiyopungua kidato cha sita. Kazi hiyo ina majukumu makubwa yanayohitaji upeo na uelewa na uwezo wa kusoma na kutafiti masuala mengi.
Kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais, kinga ya Rais kushtakiwa
Fursa hii iwekwe ili kumsaidia mtu kujibidisha katika uadilifu na uwajibikaji tangu aingiapo madarakani hadi anapotoka. Kuhoji matokeo inasaidia kuondoa manung’uniko ya wale walioshindwa na kurejeshea wananchi imani kwa aliyeshinda.
Baraza la Wazee
Kuwe na Baraza la Wazee lenye uwakilishi wa Kanda za kimila (cultural zones) na Taasisi mbali mbali zinazosimamia maadili (kama za dini). Baraza liwe pia na uwakilishi wa sehemu za jamii kama wanaume na wanawake na liwe la kushauri na kuamua au kuafiki kuhusu mambo muhimu yanayohusu maadili, mila na uhai wa Taifa. (Vilevile ikiwa nchi imeingia vitani liweze kuafiki kama iendelee na vita au la).
NAMNA YA KUSHIRIKI MCHAKATO
Lazima kujiandaa vizuri kwa kusoma nyaraka muhimu, kuzitafakari kwa muktadha wa maisha yetu kama Watanzania ili tuweze kutoa maoni yenye hoja nzito. Tuongeze mwamko wetu na tujitokeze kwa wingi na kutoa maoni yetu. Mpango Tume una hatua hizi:
Kuundwa Tume
Utoaji wa elimu kwa umma
Kukusanya maoni :
Kazi hii imekwishaanza. Katika kila mkoa vinawekwa vituo vya mikutano hiyo. Tunaweza kutoa maoni kwa kujieleza ama kwa kuandika. Ikiwa unashindwa kufika mkutanoni, basi andika na kupeleka Tume au kutuma kwa njia ya posta au barua pepe. Maoni yanaweza kuwa ya mtu mmoja ama ya kikundi.
Kufanya majumuisho na uchambuzi
Tume itaweka maoni ya watu pamoja. Maoni yaliyotajwa na kuelezewa vizuri na wengi yatapewa uzito
Uandikaji wa Rasimu ya Katiba
    Rasimu kujadiliwa katika Mabaraza ya Katiba. Kurudisha majumulisho kwa watu kupitia Mabaraza ya Katiba
    Urutubishaji / uboreshaji wa Rasimu baada ya michango ya Mabaraza ya Katiba


    Bunge la Katiba kuijadili Rasimu
    Kura ya maoni
    Kuanza kutumika kwa Katiba mpya


Mwisho : Ikiwa itakosa kupitishwa kwa 50% mara ya kwanza kura itarudiwa. 50% ikikosekana tena, basi tutaendelea kutumia Katiba ya sasa hadi mchakato mwingine utakapoandaliwa.All the contents on this site are copyrighted ©.