2013-01-25 11:26:06

Hakikisheni kwamba, uchaguzi mkuu nchini Kenya hapo tarehe 4 Machi 2013 unakuwa huru na wa haki!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linaitaka Tume Huru ya Uchaguzi nchini Kenya, kuhakikisha kwamba, inasimamia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo tarehe 4 Machi 2013 unakuwa huru na wa haki. Maaskofu katika tamko lao lililotiwa sahihi na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, wanasema, wamesikitishwa na vitendo vya baadhi ya wanasiasa kuanzisha vurugu na uvunjifu wa amani wakati wa kupitisha majina ya wagombea wa vyama vyao hivi karibuni.

Hii ni changamoto kwa wanasiasa nchini Kenya kuhakikisha kwamba, wanazingatia utawala wa sheria na demokrasia. Bado kuna wanasiasa ambao wamejikita katika utoaji rushwa, vurugu, ubinafsi na upendeleo, mambo ambayo yanadhalilisha haki msingi za binadamu, demokrasia na utawala bora nchini Kenya. Wananchi wa Kenya wanapaswa kubadilika na kukumbatia mwelekeo mpya katika utekelezaji wa demokrasia na utawala bora nchini humo.

Kwa sasa kuna taarifa zinazoonesha vitendo ambavyo vinatishia amani na usalama wa raia, kinyume kabisa na matarajio yalioneshwa na wananchi wa Kenya katika: Katiba Mpya, Tume huru ya Uchaguzi, Mwongozo Mpya wa Vyama vya Siasa na Marekebisho makubwa yaliyofanywa katika Mahakama.

Inasikitisha kuona kwamba, wanasiasa ambao kwa siku kadhaa wamekuwa wakihubiri siasa ya demokrasia, utawala bora na sheria, sasa wamekuwa wa kwanza katika kuvunja misingi hii, kiasi cha kutishia amani na utulivu wakati wa uchaguzi mkuu hapo tarehe 4 Machi 2013. Maaskofu wanawataka wanasiasa na vyombo vya sheria, ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba, vinajenga mazingira ambayo yatahakikisha kwamba, uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini humo unazingatia: uhuru, ukweli, uwazi na amani.All the contents on this site are copyrighted ©.