2013-01-25 10:45:03

Haki na amani ni chanda na pete!


Dr. Navanethem Pillay, Kamishina wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, hivi karibuni alikutana na kuzungumza na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na kusema kwamba, haki na amani ni chanda na pete, kamwe haviwezi kutenganishwa. Viongozi hao wawili walishirikishana mang'amuzi na kazi zao katika mchakato wa kudumisha haki na amani katika Jukwaa la Kimataifa, sanjari na maandalizi ya Mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni utakaofanyika mwezi Oktoba 2013.

Dr. Pillay amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni na kwamba, Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililotolewa na Umoja wa Mataifa mara tu baada ya patashika nguo kuchanika kwenye Vita Kuu ya Pili wa Dunia, linapata chimbuko lake katika tunu msingi za maisha ya Kikristo. Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeendelea kuwa ni mdau mkuu katika kuhamasisha, kulinda na kuendeleza haki na amani sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa upande wake, Dr. Tveit amebainisha mikakati inayoendelea kutekelezwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika kupigania haki msingi za binadamu, sehemu mbali mbali za dunia, kama inavyojionesha huko Pakistani na Nigeria, nchi ambazo zimekumbwa na kinzani za kidini zinazoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Hii ni changamoto ya kudumisha haki msingi za binadamu na kwa namna ya pekee, uhuru wa kuabudu ambao unafumbata haki nyingine zote!

Dr. Pillay anakiri kwamba, Umoja wa Mataifa umeendelea kushirikiana na Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika kuhamasisha utekelezaji wa haki msingi za binadamu hata kabla ya kuundwa kwa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

All the contents on this site are copyrighted ©.