2013-01-24 11:51:35

Wasifu wa Padre Joachim Ndelianarua Minja, C.PP.S


Ufuatao ni wasifu wa Marehemu Padre Joachim Minja Ndelianaruwa, C.PP.S. Bwana Iongoze miguu yetu katika njia ya amani, ndiyo iliyokuwa kauli mbiu ya maisha na utume wa Kimissionari na Kipadre ndani ya Shirika la Wamissionari Wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania. Marehemu Pd. Joachim alizaliwa mnamo tarehe 14/04/1966 – MARANGU, MOSHI, Parokia ya MARANGU - MAKOMU, Moshi Vijijini, Jimbo Katoliki la Moshi.
Ni mtoto wa Mzee Ignasi Ndesingo Lemnge na Mama Maristella Ngelyakyau. Alibatizwa tarehe 9 Mei 1966 Parokia ya Marangu, Makomu, Jimbo Katoliki Moshi. Akapata Komunyo ya kwanza hapo tarehe 26 Machi 1978, Parokiani Marangu na Kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara hapo tarehe 23 Novemba 1978 katika Parokia ya Mbahe, Arisi, Jimbo Katoliki Moshi.
ELIMU YA MSINGI: Shule ya msingi Komalyangoe iliyopo Marangu, Moshi, Mwaka 1976 - 1982.
ELIMU YA SEKONDARI; Sekondari ya LAKE iliyopo Mwanza – 1983 – 1986. Na kidato cha Tano na Sita katika Sekondari ya Mzumbe iliyopo Morogoro kati ya mwaka 1987 - 1989.
Malezi ya wito wa Kimissionari na Kipadre
Marehemu Padre Joachim Ndelianaruwa alilifahamu Shirika akisoma Mzumbe Morogoro na akapata nafasi ya kuhudhuria semina ya wito iliyoendeshwa na mlezi wa miito pale Bigwa Unitas – Morogoro mwaka 1987. Mnamo mwaka 1991 alijiunga na nyumba ya malezi Miyuji – Dodoma kwa malezi ya kwanza.
Mwaka 1992 hadi mwaka 1994 alisoma Falsafa katika Seminari kuu ya Kibosho iliyopo Jimbo la Moshi. Mwaka 1994 hadi 1995 – alirudi Dodoma katika nyumba ya malezi kwa ajili ya mwaka wa pili wa Malezi. Mnamo mwaka 1995 hadi 1998 alipelekwa Morogoro kwa ajili ya masomo ya Taalimungu.
Kunako tarehe Mosi Mei, 1997 alipewa huduma ya Usomaji Altareni na Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki, Morogoro. Tarehe 2 Mei 1998 akapata huduma ya Utumishi wa Altare, kwenye nyumba ya Malezi, Miyuji, Jimbo Katoliki Dodoma. Alipelekwa Mwaka wa mazoezi ya kichungaji, Parokia ya Itigi, Jimbo Katoliki Singida kati ya Mwaka 1998 – 1999.
Marehemu Padre Joachim Ndelianaruwa alipokelewa Shirikani, Rasmi na Daima katika SHIRIKA LA WAMISIONARI WA DAMU TAKATIFU YA YESU, tarehe 21/10/1999 na Hayati Padre Antonio Calabrese, C.PP.S., katika Seminari ya Mt. Gaspar Del Bufalo – Morogoro. Alipata daraja la ushemasi wa mpito 12/12/1999 mikononi mwa Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro.
Marehemu Pd. Joachim alipewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 07/07/2000 katika nyumba ya Shirika iliyoko ALBANO LAZIALE - Roma, Italia na MWADHAMA POLYCARP KARDINALI PENGO, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la DAR ES SALAAM. Marehemu Padre Joachim Ndelianaruwa akaadhimisha Misa yake ya Shukrani tarehe 16/08/2000 katika Parokia ya Marangu – Makomu, Jimbo Katoliki Moshi.
UTUME.
Kati ya Septemba 1999 mpaka Novemba 2001 akafanya utume wake kama Paroko msaidizi – Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi Mtongani, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Kati ya Novemba 2001 mpaka Juni 2002 akafanya utume kama Msaidizi wa Procurator - Vikarieti ya Tanzania
Kati ya Juni 2002 mpaka Juni 2006 akachagulia kuwa Mchumi wa Vikarieti ya Tanzania.
Kati ya Juni 2006 mpaka Juni 2010 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika Vikarieti ya Tanzania.
Kati ya Juni 2010 mpaka anafikwa na mauti Januari 22, 2012 alikuwa akifanya utume katika Parokia na Kituo cha Hija cha Mtakatifu Gaspari del Bufalo, Mbezi Beach, Jimbo Kuu la Dar Es Salaam. Pia alikuwa akisoma shahada ya kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Tawi la Dar Es Salaam.
UGONJWA: Tarehe 20.01.2013 alianza kujisikia (Vibaya kiafya) akiumwa baada ya huduma za Jumapili ( aliadhimisha misa mbili ya kwanza na ya pili) baada ya huduma za kichungaji alikwenda kuangalia afya na alipata huduma za kimaabara - (katika Dispensari ya Dr Hiza) na aligundulika kuwa na ugonjwa wa Malaria na kuanza kutumia dawa za kutibu ugonwa huo.
UMAUTI: umauti ulimfik Pd. Joakim Ndelianaruwa siku ya Jumanne saa 12:10-15 asubuhi Tarehe 22.01.2013, katika nyumba ya Mapadre Mbezi Beach.
UCHUNGUZI WA KITAALAMU: Baada ya Kifo chake uchunguzi ulifanyika na kuonesha kuwa alikuwa pia akisumbuliwa na homa ya mapafu kitaalamu PNEUMONIA. Hivyo pamoja na shida ya malaria vikasababisha kifo chake. APUMZIKE KWA AMANI. AMINA
”LAKINI TUNA HAZINA HII KATIKA VYOMBO VYA UDONGO”. Maneno haya yapatikana katika kadi yake ya upadrisho.

Raha ya milele umpe Ee Bwana na mwanga wa milele umwangazie. Apumzike kwa amani. Amina.
FR. REGINALD MROSSO, C.PP.S – MKUU WA SHIRIKA - VIKARIETI YA TANZANIA. 24/01/2013









All the contents on this site are copyrighted ©.