2013-01-24 08:49:45

Tarehe 27 Januari 2013 Siku ya 5 Kimataifa kwa ajili ya kuombea Amani Nchi Takatifu


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013 anawalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani duniani, kwani amani ni jina jipya la maendeleo kama alivyowahi kusema Papa Paulo wa Sita, muasisi wa Siku ya Kuombea Amani Duniani.

Jumapili ijayo, tarehe 27 Januari 2013, Waamini na watu wenye mapenzi mema katika miji elfu tatu, watakusanyika kusali kwa ajili ya kuombea amani katika Nchi Takatifu. Hii itakuwa ni Siku ya Tano ya Kuombea Amani Nchi Takatifu, changamoto inayofanyiwa kazi na Vyama vya Vijana Wakatoliki, sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwachangamotisha watu wengi zaidi kujitokeza katika mchakato wa kujenga na kuimarisha amani ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo pia inamwajibisha mwanadamu. Kuna haja ya kumaliza kinzani na migogoro inayopelekea ukosefu wa misingi ya haki, amani na utulivu huko Mashariki, kwa kujikita katika mchakato wa amani na upatanisho, mambo msingi wakati huu.

Waandaaji wa Siku ya Kimataifa kwa ajili ya kuombea Amani katika nchi Takatifu wanasema kwamba, kitendo hiki kimekuwa ni kielelezo makini cha watu wanaotamani kuona kwamba, haki, amani, upendo na mshikamano vinatawala katika mioyo ya watu, badala ya kuendekeza chuki, uhasama na wivu usiokuwa na faida.All the contents on this site are copyrighted ©.