Siku ya Saba ya Kuombea Umoja wa Wakristo: kutembea katika mshikamano!
Katika siku hii ya saba ya kuombea Umoja wa Wakristo, wazo letu kuu ni kutembea katika
mshikamano. Kwenda kwa unyenyekevu na Mungu maana kutembea katika mshikamano na wote
ambao wanapambana kwa bidii kuleta haki na amani. Hii inawapa changamoto
wote ambao wanasali kuombea umoja wa kanisa wiki hii kujiuliza: Je, umoja tunaoutafuta
ni kitu gani? Tume ya Imani na Madaraja, ambayo ni pamoja na wanachama wa Baraza la
Makanisa Ulimwenguni likiwemo pia Kanisa Katoliki, inauelewa umoja kama umoja unaoonekana
katika imani moja na katika ushirika mmoja wa Ekaristi. Umoja huu wa kiekumene,
umejitolea kwa ajili ya kuvishinda vikwazo vya kihistoria na vya sasa vinavyowagawanya
Wakristo, lakini unafanya hivyo ukitazama umoja huu unaoonekana unaounganisha asili
na utume wa kanisa katika huduma kwa watu ikishinda madhara yanayoweza kutokea kumdhalilisha
mtu na kutusambaratisha. Kama Tume ilivyosema: Kanisa, linaitwa na lina mamlaka
ya kushiriki mateso ikiwatetea na kuwatunza maskini, wahitaji, na waliotengwa. Hii
inahitaji kuainisha na kuziweka wazi miundo na kuzibadili. Kazi hii ya ushuhuda ni
ya wakristu wote. Lazima kujitolea kwa ajili ya Injili hata kama kuna mateso. Kanisa
linaitwa kuponya na kupatanisha mahusiano mabovu. Linaitwa kuwa chombo cha upatanisho
katikati ya migawanyiko na chuki wanayosababisha watu. Hii ndiyo asili na kazi ya
Kanisa.
Kuna mifano mingi ya vitendo hivyo wa uponyaji na upatanisho katika
makanisa yetu. Mifano inayotukumbusha hali za dhuluma na namna ya kupambana nayo hasa
zile zinazowakandamiza wanawake. Hata katika Biblia tunaona mfano wa binti ya Zelophehad
ambaye Musa alimuomba Mungu ili apewe haki zake. Wanyonge wanayo haki ya kudai kujaliwa
na kutunzwa. Mfano mzuri wa Kanisa likiwa limeungana pamoja na wanaonewa ni mfano
alioutoa Yesu wa msamaria mwema. Msamaria mwema akiwa mtu anayewakilisha Jamii iliyotengwa
lakini anaweza kumsaidia mhitaji. Anakuwa ni chanzo cha matumaini na faraja ya kienjili.
Kutembea kwa pamoja kikristo hakuwezi kutenganishwa na kutembea kwa unyenyekevu na
Mungu tukitafuta haki, ukarimu na wema.
SALA Mungu Mtakatifu katika nafsi
tatu kwa njia ya maisha yako unatupa mfano wa pekee wa kukutegemea, wa upendo na
mshikamano. Utuunganishe tuishi namna hii. Tufundishe kushiriki matumaini tunayoyakuta
ndani ya watu wanaopambana katika maisha duniani kote. Tunaomba uvumilvu wao utuhamasishe
kushinda mgawanyiko ili tuishi tumepatana sisi kwa sisi na kutembea pamoja kwa umoja.
Mungu wa uzima tuongoze kwenye njia ya haki na amani. Amina.
MASWALI Ni
akina nani katika jamii yako wanahitaji mshikamano wa Jumuiya ya Kikristo? Ni
Makanisa gani yamekuwa na mshikamano na wewe?
Ni kwa njia umoja unaoonekana
wa Wakristo unaimarisha mshikamano wa umoja wa Kanisa kwa wale wanaohitaji haki, ukarimu
na wema katika mazingira yako? Tafakari hii imeandaliwa na Padre Emmanuel Nyaumba.